• HABARI MPYA

  Jumamosi, Oktoba 20, 2018

  MO DEWJI APATIKANA AKIWA SALAMA, JAMAA WALIMTELEKEZA GYMKHANA BAADA YA KIBANO CHA POLISI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  JESHI la Polisi nchini limefanikiwa kumpata mfanyabiashara bilionea, Mohammed ‘Mo’ Dewji aliyetekwa na watu ambao bado hawajajulikana Oktoba 11 mjini Dar es Salaam. 
  Mo Dewji amepatikana akiwa ametelekezwa katika eneo la Gymkhana mjini Dar es Salaam, lakini akiwa salama kabisa, ingawa ameonekana amedhoofu kidogo. 
  “Naomba nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini naomba nimshukuru Mheshimiwa Rais (Dk. John Pombe Joseph Magufuli) na Jeshi la Polisi, mimi ni mzima nawashukuru Watanzania wote kwa kuniombea,” amesema Mohammed ‘Mo’ Dewji aliyetekwa na watu ambao bado hawajajulikana Oktoba 11 mjini Dar es Salaam. 
  Mo Dewji amepatikana ndani ya saa 24 tu, tangu Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro awaoanyeshe Waandishi wa habari gari inayosadikiwa kutumika katika utekaji huo.

  Mohammed ‘Mo’ Dewji aliyetekwa Oktoba 11 mjini Dar es Salaam amepatikana usiku wa kuamkia leo 

  Juzi Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Simon Sirro leo aliwaonyesha Waandishi wa Habari picha za gari ambalo lilihusika katika tukio la utekaji wa Mo Dewji, Oktoba 11 mwaka huu katika Hotel ya Colosseum Jijini Dar es Salaam.
  “Utaona ni (gari) aina ya Surf, na wakati ule wa asubuhi ulikuwa unaona kama  black (nyeusi), na ukiona chini kwenye ufito wa chini wenzetu ambao walikuwa kwenye tukio wanatambua kwamba ni gari ya namna hiyo,”alisema IGP Simon Sirro wakati akiwaonyesha Waandishi wa Habari picha hizo.
  Katika mfululizo wa uchunguzi wake, Polisi iliwatia nguvuni watu 26, kabla ya kuwaachia kwa dhamana 20 kati yao akiwemo Msemaji wa klabu ya Simba SC, Hajji Sunday Manara.
  Na hiyo ilifuatia Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola kulitaka Jeshi hilo kuharakisha upelelezi wake ili lisiwashikilie washukiwa kwa zaidi ya saa 24. 
  Aidha, watu hao waliachiwa baada ya familia ya Mo Dewji kutangaza zawadi ya Shilingi Bilioni 1 yeyote atakayesaidia kupatikana kwa mpendwa wao huyo aliyetekwa Oktoba 11, mwaka huu.
  Baba mdogo wa Mo Dewji, Azim Dewji ambaye pia ni mfadhili wa zamani wa Simba SC, alitoa ofa hiyo mapema wiki hii katika mkutano na Waandishi wa Habari jengo la Golden Jubilee Towers ghorofa ya 20 mtaa wa Ohio, Posta mjini Dar es Salaam.
  Dewji alisema kwamba Mwenye taarifa anaweza kuwasiliana na mwanafamilia, Murtaza Dewji kwa namba 0755030014, 0717208478, 0784783228 na email ya findmo@metl.net.
  Dewji mwenye umri wa miaka 43 alitekwa asubuhi ya Oktoba 11, mwaka huu akiwa anaingia katika gym ya Collessium eneo la Masaki mjini Dar es Salaam kufanya mazoezi baada ya watu wasiojulikana kufyatua risasi hewani mfululizo wakati bilionea huyo anateremka kwenye gari yake kabla ya kumbeba na kumpakia kwenye gari lao na kutokomea naye kwa kasi.
  Mohammed, mtoto wa mfanyabiashara wa siku nyingi, Gulamabbas Dewji – ni rais wa makampuni MeTL Group yaliyoasisiwa na baba yake huyo ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Singida Mjini kwa tiketi ya CCM kati ya mwaka 2005 na 2015. 
  Februari mwaka huu ilielezwa utajiri wa Dewji unafikia dola za Kimarekani Bilioni 1.5 hivyo kushika nafasi ya 17 katika orodha ya matajiri wa Afrika na kuwa mfanyabiashara kijana tajiri zaidi.
  Kwa sasa, Mo Dewji yuko mbioni kuwa mmiliki wa klabu ya Simba kufuatia mkutano wa wanachama wa Desemba 3, mwaka jana kuazimia kumfanya bilionea huyo kuwa mwanahisa mkuu katika mfumo mpya wa uendeshwaji.
  Siku hiyo, Dewji alikubali kununua asilimia 49 za hisa za klabu ya Simba SC kulingana na maelekezo ya Serikali badala ya asilimia 51 alizotaka yeye mwenyewe awali. 
  Ikumbukwe Mo pekee aliweka dau la Sh Bilioni 20 kuomba asilimia 50 ya hisa, baada ya klabu kutangaza kuuza asilimia 50 ya hisa zake kwa Sh. Bilioni 20 miezi miwili iliyopita, ingawa baadaye Serikali ikaagiza klabu hiyo isiuze zaidi ya asilimia 49 kwa mtu mmoja.
  Wanachama 1320 walihudhuria mkutano huo wa Desemba 3, mwaka jana kutoka Dar es Salaam na mikoa jirani na kwa furaha ya ushindi huo, Mo Dewji alitoa ahadi 10 za kuleta mabadiliko makubwa, ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa mazoezi wa nyasi za asili na nyasi bandia pamoja na hosteli ya kisasa ya wachezaji.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MO DEWJI APATIKANA AKIWA SALAMA, JAMAA WALIMTELEKEZA GYMKHANA BAADA YA KIBANO CHA POLISI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top