• HABARI MPYA

  Alhamisi, Oktoba 25, 2018

  KOCHA WA YANGA, MWINYI ZAHERA AWABADILISHIA MBINU KMC ILI AWAPE ADHABU SAWA YAO LIGI KUU TAIFA LEO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM 
  KOCHA Mkuu wa Yanga SC, Mwinyi Zahera amesema kwamba anatarajia ushindani kutoka kwa KMC pamoja na ugeni wao kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa sababu wana timu nzuri.
  Zahera alisema hayo jana kuelekea mchezo wa leo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya KMC unaotarajiwa kuanza Saa 1:00 usiku Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam. 
  “Tumejiandaa vyema kama ambavyo huwa tunajiandaa michezo mingine kikubwa ni kwamba tutaingia uwanjani na kucheza kwa aina ya tofauti kidogo kutokana na timu ambayo tunacheza nayo, KMC ni timu iliopanda ligi kuu msimu huu ila siwezi wabeza maana wana mwalimu na wachezaji wazuri pia,” amesema Zahera.

  Kocha Mkuu wa Yanga SC, Mwinyi Zahera (katikati) aiwa na Msaidizi wake, Mzambia Noel Mwandila na Mratibu wa timu, Hafidh Saleh 

  Ligi Kuu inatarajiwa kuendelea leo na mbali na KMC na Yanga, Mbeya City nao watakuwa wenyeji wa Mwadui FC ya Shinyanga Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya Saa 8:00 mchana, Stand United wakiwakaribisha Mtibwa Sugar ya Morogoro Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
  Mechi nyingine Ndanda FC watawakaribisha Biashara United ya Mara Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, Mbao FC wakiwa wenyeji wa  Lipuli FC ya Iringa zote Saa 10:00 jioni.
  Na hiyo ni baada ya jana, mabingwa watetezi, Simba SC kuichapa Alliance FC ya Mwanza 5-1 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, mabao yake yakifungwa na Mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi mawili, beki Mghana, Asante Kwasi, mshambuliaji chipukizi wa Kitanzania, Adam Salamba na kiungo Mzambia, Clatous Chama, huku la wageni likifungwa na Zabona Khamis. 
  Mechi nyingine za jana, bao pekee la Yahya dakika ya 53 likaipa Azam FC ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, JKT Tanzania Uwanja wa Meja Isamuhyo huko Mbweni mjini Dar es Salaam, Lipuli FC ikaichapa 3-1 Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
  Mabao ya Lipuli yamefungwa na Issa Rashid dakika ya tisa, Zawadi Mauya dakika za 14 na 39, wakati la Mbao FC limefungwa na Said Khamis Jr. dakika ya 76 kwa penalti.
  Coastal Union ikalazimishwa sare ya 1-1 na Kagera Sugar Uwanja wa Mkwakwani, Tanga wenyeji wakitangulia kwa bao la Mohammed Mussa dakika ya pili kabla ya David Luhende kuwasawazishia wageni dakika ya 22.  
  Ruvu Shooting nayo iliichapa Singida United mabao 3-1  Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, huku Tanzania Prisons ikiendelea kusuasua baada ya kulazimishwa sare ya 0-0 na African Lyon Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KOCHA WA YANGA, MWINYI ZAHERA AWABADILISHIA MBINU KMC ILI AWAPE ADHABU SAWA YAO LIGI KUU TAIFA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top