• HABARI MPYA

  Thursday, October 25, 2018

  SERIKALI YACHANGISHA FEDHA TAIFA STARS IKAWEKE KAMBI AFRIKA KUSINI KUJIANDAA NA LESOTHO KUFUZU AFCON

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SERIKALI imetangaza harambee ya kuichangia Taifa Stars ikaweke kambi Afrika Kusini kujiandaa na mchezo ujao wa kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2019 dhidi ya Lesotho mjini Maseru katikati ya mwezi ujao.
  Akizungumza na Waandishi wa Habari leo katika mkutano uliofanyika mjini Dar es Salaam, Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amewaomba wananchi na makampuni kujitokeza kuchangia kufanikisha maandalizi hayo.
  “Tunawashukuru wote waliochangia katika safari ya Cape Verde, bado tunawaomba mchango wao wa hali na mali kuelekea mchezo wa Lesotho. Gharama za kusafirisha timu yetu ya Taifa, Taifa Stars zimeongezeka zaidi ya bajeti ya awali kutokana na kambi ya nje ya nchi ambayo itakuwa Afrika Kusini,”.
  “Kwa kushirikiana na TFF Tunafanya mazungumzo na mashirika ya Ndege ili kupata bei nzuri Watanzania wengi waweze kusafiri ikiwemo mazungumzo na kampuni za mabasi kwa wale watakaosafiri kwa njia ya barabara,”amesema Waziri Mwakyembe.

  Nahodha Mbwana Samatta (kulia) atakosekana kwenye mchezo na Lesotho anatumikia adhabu ya kadi za njano 

  Aidha, Waziri Mwakyembe amesema Wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na TFF watahakikisha Taifa Stars inapata kambi nzuri nchini Afrika Kusini na salama kuelekea mchezo dhidi ya Lesotho.
  Baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Cape Verde Oktoba 16 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, Taifa Stars sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi L kuwania tiketi ya Cameroon mwakani, ikifikisha pointi tano baada ya kucheza mechi nne, ikifungwa moja na sare mbili. 
  Uganda ambayo siku hiyo iliifunga tena Lesotho 2-0 mjini Maseru, ndiyo inaongoza kundi hilo kwa pointi zake 10 za mechi nne, wakati Cape Verde inabaki na pointi zake nne katika nafasi ya tatu. Lesotho ndiyo inashika mkia kwa pointi zake mbili.   
  Taifa Stars itasafiri kuifuata Lesotho Novemba 18 mjini Maseru kabla ya kukamilisha mechi za Kundi L kwa kumenyana na Uganda Machi 22 mwakani, miezi miwili tu kabla ya kuanza kwa AFCON ya mwakani.
  Katika mchezo huo, Taifa Stars itamkosa Nahodha wake, Mbwana Ally Samatta ambaye atakuwa anatumia adhabu ya kadi mbili za njano.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SERIKALI YACHANGISHA FEDHA TAIFA STARS IKAWEKE KAMBI AFRIKA KUSINI KUJIANDAA NA LESOTHO KUFUZU AFCON Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top