• HABARI MPYA

  Ijumaa, Oktoba 19, 2018

  AZAM FC YABURUDIKA KILELENI LIGI KUU BAADA YA KUIPIGA AFRICAN LYON 2-1, NDANDA NA MWADUI ZABANWA NYUMBANI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU ya Azam FC imejitanua kileleni mwa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya African Lyon usiku wa leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam.
  Pongezi kwa beki Abdallah Kheri aliyeifungia bao la ushindi Azam FC dakika ya 89 akimalizia kona maridadi iliyochongwa na mshambuliaji Yahya Zayed.
  Na Azam FC ililazimika kutoka nyuma kupata ushindi huo, kwani Mganda Hood Mayanja alitangulia kuifungia African Lyon dakika ya nane baada ya kuanzishiwa kona fupi na kufumua shuti lililombabatiza Mudathir Yahya Abbas kabla ya kumpita kipa Mghana, Razack Abalora.

  Azam FC imejitanua kileleni mwa Ligi Kuu baada ya ushindi wa 2-1 leo

  Na alikuwa Yahya Zayed aliyeisawazishia Azam FC dakika ya 13 kwa shuti kali akiunganisha krosi nzuri ya kiungo Joseph Mahundi.
  Kwa ushindi huo, Azam FC imefikisha pointi 21 baada ya kucheza mechi tisa, ikifuatiwa na Mtibwa Sugar pointi 17 mechi tisa, Yanga SC pointi 16 mechi sita, Singida United pointi 16 mechi tisa na Simba SC pointi 14 mechi saba.
  Katika mechi nyingine zilizochezwa leo, Mwadui FC imelazimishwa sare ya bila kufungana na Ruvu Shooting Uwanja wa Mwadui Complex sawa na Ndanda FC ambayo pia imetoka 0-0 na Mbeya City Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara. 
  Ligi Kuu itaendelea kesho kwa mechi tatu, Tanzania Prisons wakianza na Singida United ya Singida Saa 8:00 mchana Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Coastal Union na JKT Tanzania ya Dar es Salaam Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga na Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, Yanga SC watakuwa wenyeji wa Alliance FC ya Mwanza. 
  Mechi nyingine tatu zitafuatia Jumapili, mabingwa watetezi, Simba SC wakiwakaribisha Stand United Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, Lipuli FC wakiwakaribisha Kagera Sugar ya Bukoba Saa 8:00 mchana Uwanja wa Samora mjini Iringa na Mbao FC wakiwa wenyeji wa Mtibwa Sugar ya Morogoro Saa 10: 00 jioni Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC YABURUDIKA KILELENI LIGI KUU BAADA YA KUIPIGA AFRICAN LYON 2-1, NDANDA NA MWADUI ZABANWA NYUMBANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top