• HABARI MPYA

  Monday, October 29, 2018

  SAMATTA AFUNGA BAO BADO KIDOGO GENK ISHINDE, IKASAWAZISHIWA DAKIKA YA MWISHO NA KUTOA SARE 1-1 UGENINI

  Na Mwandishi Wetu, LIEGE
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta jana alifunga bao lililoelekea kuipa ushindi timu yake, KRC Genk kabla ya kusawazishiwa dakika ya mwisho na kutoa sare ya 1-1 na wenyeji, Standard Liege katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Maurice Dufrasne mjini Liege.
  Samatta alianza kufunga dakika ya 84 akimalizia pasi ya kiungo Mspaniola, Alejandro Pozuelo Melero, lakini Genk wakafanya uzembe na kuwaruhusu wenyeji kusawazisha dakika ya pili ya muda wa nyongeza baada ya kutimia dakika 90 kupitia kwa beki Christian Luyindama Nekadio kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  Pamoja na sare hiyo, Genk inabaki juu kwenye msimamo wa Ligi ya Ubelgiji ikifikisha pointi 30 baada ya kucheza mechi 12, ikfuatiwa na Club Brugge inayoshika nafasi ya pili kwa pointi zake 27 za mechi 12.
  Mbwana Samatta (kushoto) akiifungia Genk bao lililoelekea kuwa la ushindi jana 
  Mbwana Samatta (kulia) akipongezwa na na mchezaji mwenzake wa Genk bao jana 

  Kwa Samatta jana amefikisha mechi 125 katika mashindano yote tangu amejiunga na Genk Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na amefunga jumla ya mabao 48.
  Katika Ligi ya Ubelgiji amecheza mechi 97 na kufunga mabao 34, Kombe la Ubelgiji mechi nane mabao mawili na Europa League mechi 20 mabao 14.
  Kikosi cha Standard Liege kilikuwa; Ochoa, Cimirot, Emond, Carcela, Marin, Djenepo/Sa dk82, Fai, Luyindama, Bastien/Lestienne dk68, Cavanda na Laifis.
  KRC Genk : Vukovic, Maehle, Aidoo, Lucumi/Dewaest dk21, Uronen, Heynen, Malinovskyi, Pozuelo, Piotrowski/Paintsil dk45, Ndongala/Fiolic dk82 na Samatta.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SAMATTA AFUNGA BAO BADO KIDOGO GENK ISHINDE, IKASAWAZISHIWA DAKIKA YA MWISHO NA KUTOA SARE 1-1 UGENINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top