• HABARI MPYA

  Jumanne, Oktoba 23, 2018

  AZAM FC NA JKT RUVU; VITA INAYOENDELEA KESHO JENERALI ISAMUHYO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BAADA ya kucheza mechi nne nyumbani, Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itakuwa ugenini kuvaana na JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) utakaofanyika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam.
  Azam FC inaenda kucheza na JKT ikiwa na ari kubwa baada ya kushinda mechi tatu mfululizo huku ikivuna pointi 10 kati ya 12 katika mechi nne zilizopita, hadi sasa ikiwa kileleni kwa pointi zake 21 baada ya kucheza mara tisa, ikishinda sita, sare tatu na kutopoteza hata mmoja.
  Wapinzani wao JKT Tanzania wanaofundishwa na Bakari Shime, nao hawajapoteza mchezo wowote hadi sasa ikiwa nafasi ya tisa kwenye msimamo na pointi zake 15, ikishinda mechi tatu na kutoka sare sita.
  Kocha Msaidizi wa Azam FC, Juma Mwambusi, ameweka wazi kuwa wamekiandaa vema kikosi chao kwa ajili ya kupata matokeo mazuri kwenye mchezo huo huku akidai wanawafahamu vilivyo wapinzani wao.

  Aliyekuwa mshambuliaji wa Azam FC, Kipre Tchetche (kulia) akiwatoka mabeki wa JKT Ruvu msimu wa 2014-2015 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam


  Kuelekea mchezo huo, Azam FC inatarajia kumkosa kiungo wake na Nahodha Msaidizi, Frank Domayo ‘Chumvi’, ambaye anasumbuliwa na majeraha ya goti akitarajia kukosekana kwa miezi minne huku pia Nahodha Agrey Moris, akiwa mgonjwa akitarajiwa kutokuwa sehemu ya mechi hiyo.
  Wachezaji wengine watakaokosekana ni beki David Mwantika na washambuliaji Mbaraka Yusuph na Wazir Junior, ambao wote nao ni majeruhi.
  Kiungo wake mshambuliaji, Tafadzwa Kutinyu, aliyekuwa kwenye majukumu ya timu yake ya Taifa Zimbabwe tayari ameshajiunga na wenzake mazoezini tayari kwa maandalizi ya mchezo huo.
  Huo utakuwa ni mchezo wa 19 timu hizo kukutana kwenye ligi hiyo, kwa mara ya kwanza zilikutana Septemba 6, 2008 ukiwa ni msimu wa kwanza tokea Azam FC ipande daraja, ilishuhudiwa JKT Ruvu ikishinda mabao 2-1 huku pia wakipata ushindi kama huo kwenye mechi ya mzunguko wa pili.
  Katika mechi 18 zilizopita, Azam FC imeonekana kuwa na wastani mzuri wa kushinda mechi nyingi pamoja na mabao mengi dhidi ya JKT Tanzania, imeshinda mara 10, ikafungwa tatu huku nne zikiisha kwa sare.
  Jumla ya mabao 47 yamefungwa katika mechi hizo 18, ukiwa ni wastani wa kufungwa mabao 2.6 kwenye kila mechi, Azam FC imefunga robo tatu kati ya hayo ikiweka nyavuni 33 huku JKT Tanzania yenyewe ikitupia 14 tu.
  Hii ni mara ya kwanza kwa timu hizo kukutana tokea JKT Tanzania ibadilishe jina kutoka JKT Ruvu Stars hadi jina hilo la sasa na Azam FC nayo kuwa rasmi kampuni msimu huu ikijulikana kama Azam FC Company Limited, pia matajiri hao watacheza kwa mara ya kwanza kwenye uwanja huo mpya wa maafande hao.
  Mchezo wa mwisho kukutana timu hizo ilikuwa ni Aprili 15 mwaka jana kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na kuisha kwa sare ya mabao 2-2, Azam FC ikifunga kupitia kwa wachezaji wa zamani wa timu hiyo, Shaaban Idd alitimkiwa CD Tenerife ya Hispania na Erasto Nyoni anayecheza Simba hivi sasa.

  Beki wa Azam FC, Shomary Kappmbe akiruka daluga za mchezaji wa JKT Ruvu, Haruna Adolph msimu wa 2014-2015 

  REKODI YA AZAM FC NA JKT TANZANIA LIGI KUU;
                           P  W  D  L GF GA  GD  Pts
  Azam FC         18 10  5  3  33  14     19   35
  JKT Tanzania  18  3    5 10  14  33   -19  14
  MECHI ZILIZOPITA AZAM FC NA JKT TANZANIA TANGU TIMU HIYO INAITWA JKT RUVU
  15.04.2017            JKT Tanzania – Azam FC          2 – 2
  22.10.2016            Azam FC – JKT Tanzania           1 – 0 
  04.05.2016           Azam FC – JKT Tanzania            2 – 2
  29.10.2015           JKT Tanzania – Azam FC            2 – 4
  07.03.2015           JKT Tanzania – Azam FC            0 – 1
  25.10.2014           Azam FC – JKT Tanzania            0 – 1
  19.04.2014           JKT Tanzania – Azam FC             0 – 1
  13.10.2013           Azam FC – JKT Tanzania             3 – 0
  20.02.2013           JKT Tanzania – Azam FC             0 – 4
  28.09.2012           Azam FC – JKT Tanzania             3 – 0
  01.04.2012           Azam FC – JKT Tanzania             4 – 1
  15.10.2011           JKT Tanzania – Azam FC             0 – 2
  20.02.2011           JKT Tanzania – Azam FC             0 – 2
  29.09.2010           Azam FC – JKT Tanzania             0 – 0
  18.02.2010           JKT Tanzania – Azam FC             1 – 1
  04.10.2009           Azam FC – JKT Tanzania             1 – 1
  24.01.2009           JKT Tanzania – Azam FC            2 – 1
  06.09.2008           Azam FC – JKT Tanzania            1 – 2
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC NA JKT RUVU; VITA INAYOENDELEA KESHO JENERALI ISAMUHYO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top