• HABARI MPYA

  Jumapili, Oktoba 21, 2018

  SIMBA SC YACHACHAMAA LIGI KUU, YAITANDIKA STAND UNITED 3-0 OKWI NA CHAMA WOTE WAFUNGA

  Na Sada Salmin, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC wamevuta kasi katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Stand United ya Shinyanga jioni ya leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Ushindi huo uliotokana na mabao ya kiungo Mzambia Clatous Chama, mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi na la kujifunga la beki mzawa Erick Murilo unaifanya Simba SC ifikishe pointi 17 baada ya kucheza mechi nane.
  Simba SC, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu, sasa wanazidiwa pointi mbili na mahasimu wao wa jadi, Yanga SC ambao wamecheza mechi saba na pointi nne na vinara, Azam FC waliocheza mechi tisa.
  Katika mchezo wa leo, Chama aliifungia bao la kwanza Simba SC dakika ya 31 baada ya kumlamba chenga beki wa Stand United, Jackob Massawe kufuatia kupokea pasi ya Shiza Kichuya na kufukua shuti lililomshinda kipa Mohammed Makaka.
  Wachezaji wa Simba SC wakipongezana baada ya bao la tatu leo

  Emmanuel Okwi akitafuta maarifa ya kumpita beki wa Stand United 
  Meddie Kagere akimtoka beki wa Stand United

  Okwi akafunga bao zuri la pili dakika ya 45 na ushei baada ya kupokea pasi ndefu ya Chama na kuwatoka mabeki wa Stand United kabla ya kumchambua Makaka aliyefanya kazi nzuri awali ya kuokoa michomo mingi ya hatari.
  Beki Erick Murilo akajifunga dakika ya 78 katika juhudi za kuokoa kona iliyochongwa kiungo Shiza Kichuya kuipatia Simba SC bao la tatu.
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, bao pekee la Suleiman Mangoma dakika ya 61 lilitosha kuipa ushindi wa 1-0 ugenini Kagera Sugar dhidi ya wenyeji, Lipuli FC Uwanja wa Samora mjini Iringa.  
  Nayo Mbao FC imeichapa Mtibwa Sugar ya Morogoro 1-0 bao pekee la Said Khamis dakika ya 48 Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza. 
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murshid, Pascal Wawa, Said Ndemla, Shiza Kichuya/Marcel Bonventure dk80, Clatous Chama, Mohammed ‘Mo’ Ibrahim/Hassan Dilunga dk64, Meddie Kagere/Adam Salamba dk80 na Emmanuel Okwi.
  Stand United: Mohammed Makaka, Datus Peter, Makenzi Kapinga, Majid Kimbondile, Erick Murilo, Ahmad Tajuden, Jacob Massawe, Hafidh Mussa, Juvenary Pastory/Chinonso Sabilo dk35/Jisend Mathias dk75, Alex Kitenge na Sixtus Sabilo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC YACHACHAMAA LIGI KUU, YAITANDIKA STAND UNITED 3-0 OKWI NA CHAMA WOTE WAFUNGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top