• HABARI MPYA

  Sunday, October 28, 2018

  OKWI AFUNGA HAT TRICK SIMBA SC YAISHUGHULIKIA KIKAMILIFU RUVU SHOOTING, YAIPIGA 5-0 TAIFA

  Na Sada Salmin, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI Mganda, Emmanuel Okwi ameanza kuonyesha cheche katika msimu mpya wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kufunga mabao matatu katika katika ushindi wa 5-0 dhidi ya Ruvu Shooting ya Pwani usiku wa leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Kwa ushindi huo ulionakshiwa na mabao mengine mawili ya Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere na mzawa, Adam Salamba, Simba SC inafikisha pointi 23 baada ya kucheza mechi 10, ikiendelea kuwa nyuma ya Azam FC inayoongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 27 za mechi 11.
  Okwi aliifungia Simba SC bao la kwanza dakika ya saba akimalizia krosi ya beki wa kulia, Shomari Kapombe baada ya kazi nzuri iliyofanywa na kiungo Shiza Ramadhani Kichuya.
  Emmanuel Okwi akishangilia baada ya kuifungia Simba SC mabao matatu katika ushindi wa 5-0 dhidi ya Ruvu Shooting leo
  Emmanuel Okwi akikabidhiwa mpira baada ya kuifungia Simba SC mabao matatu leo
  Mfungaji wa bao la pili Simba SC, Meddie Kagere akijaribu kumpiga chenga beki wa Ruvu Shooting leo
  Emmanuel Okwi akiwachambua wachezaji wa Ruvu Shooting leo Uwanja wa Taifa
  Kikosi cha Simba SC kilichoichapa Ruvu Shooting 5-0 leo Dar es Salaam

  Kagere akaifungia Simba SC bao la pili dakika ya 23 akimalizia mpira uliorudi baada ya kugonga mwamba kufuatia shuti la Nahodha, mshambuliaji John Raphael Bocco na hadi mapumziko mabingwa hao watetezi walikuwa wanaongoza kwa 2-0.
  Kipindi cha pili, Okwi tena akaanza kufunga dakika ya saba tangu mchezo kuanza tena, kwa mara nyingine akimalizia krosi ya Kapombe ambaye naye alipasiwa na Chama.
  Okwi, mchezaji wa zamani wa Yanga SC ya Dar es Salaam pia, akakamilisha hat trick yake dakika ya 77 akimalizia pasi ya Chama ambaye naye alipokea krosi ya Kapombe, hivyo kuwa mchezaji wa pili tu msimu huu kupiga hat trick baada ya mshambuliaji wa Stand United, Alex Kitenge.
  Kocha Mbelgiji, Patrick J. Aussems akampumzisha Okwi na kumuingiza mshambuliaji chipukizi, Adam Salamba aliyekwenda kufunga bao la tano dakika 89 akimalizia pasi ya mtokea benchi mwingine, Hassan Dilunga.
  Kikosi cha Ruvu Shooting kilikuwa; Abdallah Rashid, Abdul Mpambika, Mau Bofu, Renatus Ambroce, Tumba Sued, Zuberi Dabi, Shaaban Usala, Baraka Usala, Said Dilunga, Fully Maganga/Alinanuswe Martin dk 69 na William Patrick/Chande Magoja dk57.
  Simba SC; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murshid/Paul Bukaba dk 87, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Clatous Chama, Meddie Kagere/Hassan Dilunga dk 66, John Bocco na Emmanuel Okwi/Adam Salamba dk83.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: OKWI AFUNGA HAT TRICK SIMBA SC YAISHUGHULIKIA KIKAMILIFU RUVU SHOOTING, YAIPIGA 5-0 TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top