• HABARI MPYA

  Jumamosi, Oktoba 27, 2018

  MLINDA MLANGO PETER MANYIKA ‘JUNIOR’ ASAINI MKATABA WA MWAKA MMOJA KUJIUNGA NA KCB YA KENYA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KIPA wa kimataifa wa Tanzania, Peter Manyika amesaini mkataba wa mwaka mmoja kujiunga na Benki ya Biashara ya Kenya (KCB) ya Ligi Kuu ya Kenya.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo mjini Dar es Salaam, Manyika amesema kwamba ni furaha wake kujiunga na moja ya timu kubwa Afrika Mashariki, KCB.
  “Ninayo furaha kutamka kwamba mimi ni mchezaji wa KCB, hii ni timu kubwa Kenya na Afrika Mashariki, naelekeza nguvu zangu kwenye kuitumikia klabu hiyo kwa mafanikio,”amesema.
  Manyika amesaini mkataba huo leo mjini Dar es Salaam na viongozi wa KCB waliokuja hapa kuhakikisha wanaipata saini ya kipa huyo anayefuata nyayo sa baba yake, Manyika Peter aliyedakia klabu za Mtibwa Sugar ya Morogoro, Sigara na Yanga za Dar es Salaam pamoja na timu ya taifa, Taifa Stars. 
  Peter Manyika akifurahia baada ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja kujiunga na KCB ya Ligi Kuu ya Kenya
  Peter Manyika akisaini mkataba wa mwaka mmoja kujiunga na KCB ya Ligi Kuu ya Kenya

  Na KCB walivutiwa na Manyika baada ya kumuona akiidaikia Singida United katika michuano ya SportPesa Super Cup Juni mwaka huu mjini Nakuru nchini Kenya.
  Manyika ameidakia Singida United kwa msimu mmoja tu baada ya kujiunga nayo akitokea klabu yake ya kwanza kabisa kihistoria, Simba SC alikoanzia timu ya vijana baada ya kusajiliwa Julai mwaka 2014 kufuatia kung’ara akiwa na timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys. 
  Aliondoka Simba SC Julai mwaka 2017 baada ya kuidakia jumla ya mechi 51 za mashindano tofauti, nyingi za kirafiki akifanikiwa kusimama langoni mara 30 bila kuruhusu nyavu zake kuguswa huku akiwa amefungwa jumla ya mabao 34.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MLINDA MLANGO PETER MANYIKA ‘JUNIOR’ ASAINI MKATABA WA MWAKA MMOJA KUJIUNGA NA KCB YA KENYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top