• HABARI MPYA

    Monday, October 22, 2018

    AMMY NINJE ATEULIWA KUWA MKURUGENZI MPYA WA UFUNDI WA TFF AKICHUKUA NAFASI YA MILAMBO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KAMATI ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imemthibitisha Ammy Conrad Ninje kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa shirikisho hilo.
    Ninje anachukua nafasi ya Oscar Milambo aliyekuwa anakaimu nafasi hiyo kwa muda tangu katikati ya mwaka kufuatia Salum Madadi kubadilishiwa majukumu.
    Mchezaji huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars anapewa Ukurugenzi wa Ufundi baada ya kuwa Kocha wa timu mbalimbali za taifa za vijana na wakubwa.  
    Alianza kama Kocha Msaidizi wa Taifa Stars chini ya mzalendo mwenzake, Salum Mayanga mwaka jana kabla ya kupandishwa na kuwa kocha wa kikosi cha Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ kilichoshiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Challenge nchini Kenya mwaka jana.

    Ammy Ninje (kushoto) mara ya mwisho alikuwa kocha wa Ngorongoro Heroes akisaidiwa na Juma Mgunda na Meneja, Leopold Mukebezi 'Taso'

    Pamoja na Kilimanjaro Stars kufanya vibaya kwenye michuano hiyo, Ninje akapandishwa kuwa kocha wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes ambayo nayo haikuwa na matokeo mazuri baada ya kutolewa mapema kwenye mechi za kufuzu AFCON U20 mwakani Niger.
    Kihistoria Ammy Ninje alizaliwa mwaka 1978, Dar es Salaam, Tanzania na alianza shule msingi Bunge iliyopo Jiji Kuu la Tanzania,  kuanzia mwaka 1985 – 1991.
    Alisoma shule ya Sekondari ya Kilimanjaro 1992 na baadaye alijiunga kidato cha tano na sita Shule ya Sekondari ya Al-Haramain, Kariakoo jijini.
    Alianza kucheza soka katika timu ya Boom FC ya Ilala na baadaye Manyema FC zote za Dar es Salaam kabla ya kujiunga JKT Ruvu wakati huo inaitwa 832 KJ Ruvu.
    Baadaye alikwenda kucheza soka Afrika Kusini kwenye timu za Hellenic FC na kisha Wynberg St Jones kabla  ya kujiunga na Sparta Rotterdam (Mutual) FC ya China pia alicheza katika nchi za Denmark, USA, Scotland na England.
    Ninje, ambaye kitaalum ni Mhasibu, amewahi kucheza timu ya Taifa ya Tanzania katika vipindi tofauti wakati inafundishwa na Kocha mzawa Dk. Mshindo Msolla kabla ya kuanza kufundisha soka katika chuo cha Hull mwaka 2007 hadi 2010.
    Amefundishwa pia timu ya watoto ya shule ya Msingi ya Collingwood kati ya 2009 na 2013, Soccer kati ya 2012 na 2014, Notts County FC kati ya 2013 hadi mwaka jana aliporejea nyumbani Tanzania na kuanza kufundisha timu za taifa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AMMY NINJE ATEULIWA KUWA MKURUGENZI MPYA WA UFUNDI WA TFF AKICHUKUA NAFASI YA MILAMBO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top