• HABARI MPYA

    Saturday, April 04, 2015

    SIMBA SC NA KAGERA SUGAR ‘WAIPIGA MANDE’ SHIREFA KUAHIRISHA MECHI SABABU YA VIDIMBWI

    Na Philipo Chimi, SHINYANGA
    MCHEZO wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya wenyeji, Kagera Sugar dhidi ya wapinzani wao, Simba SC leo umeshindwa kufanyika Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga kutokana na Uwanja kuwa na madimbwi ya maji baadhi ya sehemu, baada ya mvua iliyonyesha.
    Mchezo huo kushindwa kufanyika umezua tafrani kubwa Uwanja wa Kambarage, iliyodumu zaidi ya saa mbili, viongozi wa Simba na mashabiki wa soka mkoani hapa wakitoa lawama kwa uongozi wa Chama cha Soka Shinyanga (SHIREFA) chini ya Mwenyekiti wake, Benister Lugola.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY leo mjini hapa, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya klabu ya Simba, Hajji Sunday Manara amesema kwamba kushindwa kufanyika kwa mchezo huo ni njama ya uongozi wa SHIREFA, kwani hali ya Uwanja ilikuwa nzuri mchezo kuchezwa.

    “Sisi kama Simba, tunaamini kabisa uongozi wa FA mkoa wa Shinyanga haujaanya vyema kuzuia mchezo huu, kwani wao wanacholenga ni maslahi, walihofia watu kuwa wachache uwanjani, bila kujua sisi tunatumia gharama kukaa hoteli kusubiri mchezo mwingine,”alisema Manara.
    Naye Kocha Msaidizi wa Kagera Sugar, Mlange Kambange amesema maamuzi ya SHIREFA kuahirisha mchezo huo sio mazuri, kwani wachezaji na mashabiki walikuwa na morali licha hali ya hewa kuwa mbaya.
    “SHIREFA imeamua vibaya kuahirisha mchezo, kwani sisi kama timu zote mbili tulikuwa tumekwishakubali kucheza, maana Uwanja hauna maji, japo sehemu za magoli kuna maji kidogo,” alisema Kabange.
    Kwa upande wake, Katibu wa SHIREFA, Said Nasoro alisema hali ya hewa ilikuwa hairuhusu mchezo huo kuchezwa kutokana na Uwanja kujaa maji baadhi ya maeneo, hivyo ingeathiri mchezo huo.
    Mchezo huo sasa utapigwa Jumatatu Uwanja wa Kambarage, wakati kesho Stand United itaikaribisha Mtibwa Sugar katika mchezo mwingine wa ligi hiyo Uwanja wa Kambarage.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC NA KAGERA SUGAR ‘WAIPIGA MANDE’ SHIREFA KUAHIRISHA MECHI SABABU YA VIDIMBWI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top