• HABARI MPYA

    Sunday, August 08, 2021

    MWANARIADHA WA TANZANIA, ALPHONCE FELIX SIMBU AMALIZA NAFASI YA SABA KWENYE MARATHONI MICHEZO YA OLIMPIKI TOKYO

    MWANARIADHA wa Tanzania, Alphonce Felix Simbu amemaliza nafasi ya saba kwenye mbio za Marathoni Michezo ya Olimpiki Alfajiri ya huko Sapporo, Japan, kilomita 500 kaskazini kwa Jiji la Tokyo.
    Simbu ametumia muda wa saa mbili, dakika 11 na sekunde 35, akizidiwa kwa wastani wa dakika tatu na Mkenya Eliud Kipchoge aliyeongoza na kutwaa tena Medali ya Dhahabu.
    Kipchoge ametetea vyema taji lake la Marathon na kuwa mwanariadha wa kwanza tangu mwaka 1980 kutwaa mfululizo Medali za Dhahabu za Marathoni kwenye Olimpiki na wa tatu tu kushinda mfululizo katika michezo hiyo, akitumia muda wa saa mbili, dakika nane na sekunde 38.


    Akipewa hadhi ya mwana Marathon bora wa muda wote, mkimbiaji huyo mwenye umri wa miaka 36 alimaliza dakika moja na sekunde 20 kabla ya Mholanzi Abdi Nageeye aliyechukua Fedha, wakati Mbelgiji Bashir Abdi alimshinda Mkenya mwingine, Lawrence Cherono na kuchukua Shaba.
    Wengine katika 10 Bora ni Ayad Lamdassem wa Hispania aliyeshika nafasi ya tano, Suguru Osako wa Japan nafasi ya sita, Galen Rupp wa Marekani nafasi ya nane, Othmane El Goumri wa Morocco nafasi ya tisa na Koen Naert wa Ubelgiji nafasi ya 10.
    Wanariadha wengine wa Tanzania walioshiriki Olimpiki ya Tokyo ni Gabriel Gerald Geay hakumaliza baada ya kuumia na Failuna Abdi Matanga  ameshika nafasi ya 24 upande wa wanawake.
    Yapata miaka 41 tangu Tanzania ilipotwaa kwa mara ya kwanza na ya mwisho Medali katika michezo ya Olimpiki – mwaka 1980 Jijini Moscow, Urusi kupitia kwa wanariadha Suleiman Nyambui Mujaya Mita 5000 na Filbert Bayi Sanka Mita 3000 wote wakishinda Fedha baada ya kumaliza nafasi ya pili.

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MWANARIADHA WA TANZANIA, ALPHONCE FELIX SIMBU AMALIZA NAFASI YA SABA KWENYE MARATHONI MICHEZO YA OLIMPIKI TOKYO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top