• HABARI MPYA

  Wednesday, January 16, 2019

  TAKUKURU YAIOMBA MAHAKAMA IWAHOJI TENA MALINZI NA MWESIGWA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeomba kuwachukua aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na Katibu Mkuu wake, Selestine Mwesigwa kwa ajili ya kuwahoji juu ya kesi inayowakabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu mjini Dar es Salaam.
  Ombi hilo la Takukuru ikiwakilishwa na Wakili Leonard Swai leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Wilbard Mashauri limekubaliwa na mahakama hiyo.
  “Mheshimiwa upande wa Jamhuri tunaomba kuwachukua mshitakiwa wa kwanza na wa pili kwa ajili ya mahojiano, kuna kitu tunataka kuongezea," alisema Swai.

  Hakimu Mashauri alikubali maombi hayo na kuahirisha kesi hadi Januari 21, mwaka huu ambapo shahidi wa tisa wa Jamhuri atatoa ushahidi wake.
  Malinzi, pamoja na aliyekuwa Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa na Mhasibu, Nsiande Isawafo Mwanga walipelekwa rumande Juni 29, mwaka juzi baada ya kusomewa mashitaka 28 ya kughushi na kutakatisha fedha kupitia akaunti ya shirikisho hilo iliyopo katika banki ya Stanbic, Dar es Salaam.
  Washitakiwa wengine katika kesi hiyo mbali ya Malinzi mwenye umri wa miaka 57, Mwesigwa miaka 46 na Nsia miaka 27 ni Meneja Ofisi wa TFF, Miriam Zayumba na Karani wa TFF, Flora Rauya ambao kwa pamoja wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017 na wanakabiliwa na mashitaka 30.
  Katika mashtaka hayo, Malinzi pekee anakabiliwa na mashtaka 28 ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha dola za Kimarekani 173,335 na Sh 43,100,000, wakati Mwesigwa anakabiliwa na mashitaka sita ya kula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi na utakatishaji wa fedha.
  Nsiande anakabiliwa na mashitaka mawili ya utakatishaji wa fedha, Miriam anakabiliwa na mashitaka tisa ya kughushi na Frola anakabiliwa na shitaka moja la kughushi na wote walikana mashitaka hayo.
  Malinzi, Mwesigwa na Nsiande wanaendelea kusota rumande kwa kuwa wanakabiliwa na mashtaka ya utakatishaji fedha, wakati Miriam na Flora wapo nje kwa dhamana.
  Ikumbukwe, Malinzi aliingia madarakani TFF Oktoba mwaka 2013 baada ya kupata kura 72 kati ya 126 zilizopigwa akimshinda aliyekuwa mpinzani wake wa karibu, Athumani Nyamlani.
  Hata hivyo, Malinzi alishindwa kutetea nafasi yake Agosti 12, mwaka juzi katika uchaguzi uliofanyika mjini Dodoma kutokana na kesi hiyo huku aliyekuwa Makamu wake, Wallace Karia akishinda kiti cha Urais wa shirikisho hilo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TAKUKURU YAIOMBA MAHAKAMA IWAHOJI TENA MALINZI NA MWESIGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top