• HABARI MPYA

    Sunday, January 20, 2019

    TENERIFE YAMPELEKA CHILUNDA KWA MKOPO DARAJA LA PILI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Shaaban Iddi Chilunda amejiunga na klabu ya CD Izarra yenye maskani yake Estella-Lizarra katika mji wa Navarre kutoka CD Tenerife, zote za Hispania. 
    Chilunda mwenye umri wa miaka 20, anaondoka Tenerife ya Daraja la kwanza kujiunga na Izarra iliyoanzishwa mwaka 1924, lakini inacheza Daraja la Pili, Segunda División B – Kundi la Pili, ambayo hutumia uwanja wa Merkatondoa wenye kukusanya mashabiki 3,500.
    Kwa sasa, Izarra inashika nafasi ya 14 kwenye Kundi la Pili la Segunda B lenye jumla ya timu 20 ikiwa na pointi 24 za mechi 21.



    Shaaban Iddi Chilunda amejiunga na CD Izarra ya Daraja la Pili nchini Hispania

    Chilunda alijiunga na Tenerife Agosti tu mwaka jana kwa mkopo wa miaka miwili, akitokea Azam FC ya nyumbani, Tanzania akitoka kuwa mfungaji bora wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati na kuipa taji hilo klabu yake.
    Kwa muda wake wote wa kuwa Tenerife, Chilunda amecheza dakika 29 tu katika mechi tatu, zote akiingia kutokea benchi. Na mara saba amepewa nafasi ya kukaa benchi mwanzo, hadi mwisho.
    Tenerife inamtoa Chilunda ili akapate uzoefu zaidi wa kucheza, ikiamini Izarra atakuwa anaanza kwenye mechi zote.  
    Ikumbukwe mchezaji mwenzake wa zamani wa Azam FC, Farid Mussa Malik yupo Tenerife B, inayoshiriki Ligi Daraja la Tatu ijulikanayo kama Tercera Division.
    Timu ipo katika Kundi la 12 ikiwa inashika nafasi ya sita kwa pointi zake 30 za mechi 21 na Farid kwa muda wote huo amecheza mechi tisa tu, saba akianza na mbili akitokea benchi, wakati mbili hakumaliza.
    Farid naye mwenye umri wa miaka 22 aliyejiunga na Tenerife mwaka 2016, anaweza kuondoka mwishoni mwa msimu. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TENERIFE YAMPELEKA CHILUNDA KWA MKOPO DARAJA LA PILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top