• HABARI MPYA

  Jumanne, Januari 29, 2019

  MAREFA WA SENEGAL KUCHEZESHA AL AHLY NA SIMBA JUMAMOSI MISRI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MCHEZO wa Kundi D Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya wenyeji, Al Ahly na Simba SC ya Tanzania utachezeshwa na marefa kutoka Senegal Jumamosi wiki hii Uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria.
  Hao ni Maguette Ndiaye atakayepuliza kipyenga akisaidiwa na washika vibendera Djibril Camara na El Hadji Malick Samba wakati mezani atakuwepo  Daouda Gueye.  
  Simba inashika nafasi ya tatu katika Kundi D ikiwa na pointi tatu sawa na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) inayoshika nafasi ya pili kwa wastani wake nzuri wa mabao, wakati Ahly inaongoza kwa pointi zake nne na JS Saoura ya Algeria inashika mkia kwa pointi yao moja. 

  Baada ya ushindi wa 3-0 nyumbani na kipigo cha 5-0 kutoka Vita mjini Kinshasa katika mechi zake mbili za kwanza, Simba SC inataka kwenda kuwavimbia mabingwa wa kihistoria wa Afrika, Al Ahly.
  Beki Erasto Edward Nyoni na mshambuliaji John Raphael Bocco wanatarajiwa kuendelea kukosekana kwenye kikosi cha Simba SC kutokana na kuwa majeruhi.
  Baada ya kipigo cha 5-0 kutoka kwa AS Vita, Simba ilicheza mechi tatu zaidi za michuano ya SportPesa Super Cup ikishinda 2-1 mbele ya AFC Leopards na kufungwa 2-1 na Bandari, zote za Kenya kabla ya kushinda kwa penalti 5-3 dhidi ya Mbao FC ya Mwanza.
  Mechi hizo zinatarajiwa kuwa zimempa nafasi kocha Patrick Aussems kurekebisha makosa yaliyojitokeza kwenye mechi dhidi ya AS Vita kuelekea mechi ya Jumamosi na Al Ahly.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MAREFA WA SENEGAL KUCHEZESHA AL AHLY NA SIMBA JUMAMOSI MISRI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top