• HABARI MPYA

    Monday, January 28, 2019

    AIBU ILIYOJE TANZANIA KUENDELEA KUBORONGA SPORTPESA SUPER CUP

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    ULE usemi maarufu wa Wahenga, ‘Mcheza Kwao Hutuzwa’ kwa mara nyingine umeshindwa kujidhihirisha hapa nchini kufuatia timu za Tanzania kuendelea kuboronga kwenye ardhi ya nyumbani.
    Michuano ya tatu ya SportPesa Super Cup ilifikia tamati jana kwa timu ya Kariobangi Sharks kutwaa taji hilo kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Bandari, zote za Kenya katika mchezo mzuri wa fainali uliofanyika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Pongezi kwa mfungaji wa bao pekee la ushindi Mwendwa Harrison dakika ya 61 na kwa ushindi huo, Kariobangi Sharks ya Nairobi wamezawadiwa dola za Kimarekani 30,000, zaidi ya Sh. Milioni 65 za Tanzania na pia watasafiri kwenda Uingereza kumenyana na klabu ya Everton.

    Bandari kutoka Mombasa inayofundishwa na mchezaji wa zamani wa Yanga SC, Ben Mwalala yenyewe imepatiwa dola 10,000 za Kimarekani zaidi ya Sh. Milioni 22 za Tanzania kwa kumaliza nafasi ya pili.
    Washindi wa tatu, Simba SC ambao wameifunga Mbao FC kwa penalti 5-3 baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika 90, wamepatiwa dola 7,500, zaidi ya Sh. Milioni 18 za Tanzania.
    Mbao FC wamepata dola 5,000, zaidi ya Sh. Milioni 12 za Tanzania na washiriki wengine wote, AFC Leopards, Gor Mahia na Yanga SC wamepatiwa sola 2,500 kila mmoja, zaidi ya Sh. Milioni 6 za hapa.
    Huo ni mwendelezo wa timu Kenya kutamba kwenye michuano hiyo tangu ianzishwe, mwaka 2017 Gor Mahia wakiwafunga mahasimu wao, AFC Leopards 3-0 Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam na mwaka jana wakiwafunga Simba SC 2-1 Uwanja wa Afraha mjini Nakuru.
    Katika miaka mitatu ya michuano hiyo ya wiki moja ya SportPesa Super Cup, mara mbili imefanyika Dar es Salaam na mara moja tu, mwaka jana ilifanyika nchini Kenya katika mji wa Nakuru.
    Mwaka juzi na mwaka jana michuano hiyo ilifanyika katikati ya mwaka, mara tu baada ya kalenda ya msimu ya masindano ya Tanzania.
    Lakini timu za Tanzania hazikuipa uzito michuano hiyo, zikidai wachezaji wake nyota na tegemeo wamechoka baada ya shughuli nzito ya msimu, hivyo kupeleka vikosi vilivyokosa baadhi ya nyota wake.
    Haikuwa ajabu timu za Kenya zilizoipa uzito michuano hiyo zikafanikiwa kubeba taji na kuelekea michuano ya mwaka huu, waandaaji kampuni ya SporPesa wakaamua kuirudisha nyuma hadi mwanzoni mwa mwaka, katikati kalenda ya msimu hapa nchini.
    Na bahati nzuri michuano imefanyika hapa nyumbani timu zote za Tanzania zikiwa katika moto wa kucheza Ligi Kuu na zaidi, mabingwa wa nchi Simba wao wapo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika pia.
    Ilitarajiwa msimu huu kungekuwa na matokeo tofauti kwa timu za Tanzania, lakini haikuwa hivyo, Yanga ilitolewa mapema tu katika mchezo wa kwanza wakifungwa 3-2 na Kariobangi walioibuka mabingwa na Singida United ikachapwa 1-0 na Bandari ya Kenya. 
    Simba na Bandari zenyewe baada ya kuvuka vizingiti vya awali kwa kuzitoa Gor Mahia na AFC Leopards za Kenya pia, zikaenda kukung’utwa katika Nusu Fainali na Bandari na Kariobangi.    
    Katika miaka miwili ya mwanzo sababu za kufanya vibaya kwenye michuano hiyo ni kutoipa uzito kwa kupeleka vikosi dhaifu kutokana na wachezaji nyota kuwa wamechoka baada ya mshikemshike wa msimu - mwaka huu mashindano yamekuja mapema Januari, kuna kisingizio kingine?
    Unacheza mechi tatu ndani ya wiki moja tu, ukishinda zote unapata dola za Kimarekani 30,000, ambazo ni zaidi ya Sh. Milioni 65 za Tanzania, bado nafasi ya kucheza klabu ya Everton ya England – hii ni biashara nzuri kiasi gani?
    Mwaka jana Gor Mahia walisafiri kwenda Uingereza na kucheza mechi dhidi ya Everton Uwanja wa Goodison Park, faida iliyoje kwao, baada ya mwaka wa kwanza kucheza na timu hiyo hapa Dar es Salaam. 
    Wakati umefika, viongozi wa klabu za Tanzania wajiulize baada ya mihula mitatu ya michuano ya SportPersa Super Cup kiasi gani wamepoteza fursa nzuri, wamekosa fedha na kuwaangusha wapenzi na mashabiki wa timu zao kwa kutofanya vizuri.
    Kuelekea michuano ya mwakani, ipo haja ya timu za Tanzania kujipanga vizuri na kuweka dhamira ya kufanya vyema kwenye SportPesa Super Cup ijayo.  Aibu iliyoje kwa timu za Tanzania kuendelea kuboronga michuano ya SportPesa Super Cup.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AIBU ILIYOJE TANZANIA KUENDELEA KUBORONGA SPORTPESA SUPER CUP Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top