• HABARI MPYA

  Alhamisi, Januari 31, 2019

  KICHUYA AKAMILISHA UHAMISHO WAKE MISRI, ATOLEWA KWA MKOPO ENPPI YA LIGI KUU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  WINGA wa kimataifa wa Tanzania, Shiza Ramadhani Kichuya amekamilisha uhamisho wake kujiunga na klabu ya Pharco ya mjini Alexandria nchini Misri.
  Tayari Kichuya yupo mjini Alexandria na taratibu za kumpeleka kwa mkopo klabu ya ENPPI zimekamilika na kesho ataanza mazoezi na timu yake hiyo mpya kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya Misri dhidi ya Al Ahly utakaochezwa Jumanne Februari 5.
  Pharco imeamua kumtoa kwa mkopo Kichuya ENNPI kwa sababu Ligi Daraja la Pili Misri imemalizika kwa sasa.

  Shiza Kichuya amekamilisha uhamisho wake kujiunga na Pharco ya Misri 

  Pharco iliyoanzishwa mwaka 2010 inapigana kujaribu kupanda Ligi Kuu ya Misri na msimu huu imezidiwa kete na Al Nasr Lel Taa'en, El Sharkia na Tanta zilizofanikiwa kupanda.
  Kocha wa timu hiyo, Mreno Jose Rui Lopes Aguas ambaye amejiunga na timu hiyo akitokea Cape Verde, amevutiwa mno na Kichuya baada ya kuonyeshwa uwezo wake kupitia DVD.
  Na akiwa ana umri wa miaka 22, Kichuya aliyejunga na Simba SC mwaka 2016 akitokea timu ya Mtibwa Sugar ya Morogoro anapata nafasi ya kwenda kujaribu bahati yake nje.
  Kichuya anakwenda kuunga na wachezaji wengine wawili wa Tanzania wanaocheza Ligi Kuu ya Misri ambao ni kiungo Himid Mao Mkami anayechezea Petrojet na mshambuliaji Yahya Zayd wa Ismailia, zote za Ligi Kuu na wote walikwenda huko wakitokea Azam FC.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KICHUYA AKAMILISHA UHAMISHO WAKE MISRI, ATOLEWA KWA MKOPO ENPPI YA LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top