• HABARI MPYA

  Jumanne, Januari 15, 2019

  ALLIANCE FC YALAZIMISHWA SARE NA TANZANIA PRISONS, ZATOKA 1-1 NYAMAGANA

  Na Mwandishi Wetu, MWANZA
  TIMU ya Alliance FC imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania jioni ya leo Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza.
  Na pongezi kwa mshambuliaji mkongwe, Hussein Javu aliyewika klabu za Mtibwa Sugar ya Morogoro na Yanga SC ya Dar es Salaam aliyeifungia Alliance bao la kusawazisha dakika ya 42.
  Javu anayecheza kwa mkopo Alliance FC kutoka Mtibwa Sugar, alifunga bao hilo baada ya Michael Ismail kuanza kuwafungia Tanzania Prisons dakika ya 16.
  Matokeo hayo yanayoiongezea kila timu pointi moja, yanaifanya Alliance FC ifikishe pointi 25 baada ya kucheza mechi 22 na kupanda hadi nafasi ya 11 kutoka ya 14, wakati Tanzania Prisons inafikisha pointi 16 baada ya kucheza mechi 21 na kupanda kwa nafasi moja hadi ya 19 kwenye ligi ya timu 20.

  Mchezo mwingine wa Ligi Kuu unafuatia hivi sasa kati ya wenyeji, Yanga SC dhidi ya Mwadui FC Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.  
  Yanga SC ndiyo inaongoza Ligi Kuu kwa sasa ikiwa na pointi 50 baada ya kucheza mechi 18, ikiizidi kwa pointi 10 Azam FC katika nafasi ya pili ambayo imecheza mechi 17, wakati mabingwa watetezi, Simba SC ni wa tatu kwa pointi zao 33 za mechi 14 – na Mwadui FC yenye pointi 24 za mechi 21 ni ya 11. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ALLIANCE FC YALAZIMISHWA SARE NA TANZANIA PRISONS, ZATOKA 1-1 NYAMAGANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top