• HABARI MPYA

  Jumapili, Januari 27, 2019

  SIMBA WAIPIGA MBAO KWA MATUTA NA KUSHIKA NAFASI YA TATU SPORTPRSA CUP

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MABINGWA wa Tanzania Bara, Simba SC wamefanikiwa kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye michuano ya SportPesa Super Cup baada ya ushindi wa penalti 5-3 kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam. 
  Waliofunga penalti za Simba SC ni mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi, mabeki Mghana, Nicholas Gyan, Muivory Coast, Serge Wawa, kipa mzawa Deogratias Munishi ‘Dida’ na kiungo Mzambia, Clatous Chama. 
  Kwa upande wa Mbao FC waliofunga ni Said Khamis, Peter Mwangosi na Vincent Philipo huku Rajesh Kotecha akipiga juu ya lango.

  Kikosi cha Simba SC kilichoanza dhidi ya Mbao FC leo Uwanja wa Taifa

  Kikosi cha Mbao FC kilichoibana Simba SC hadi kwenye matuta leo Uwanja wa Taifa

  Ushindi huo kwa Simba SC ni sawa ni kisasi, baada ya Septemba 20 mwaka jana Wekundu wa msimbazi kuchapwa 1-0 na Mbao FC katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
  Kipa wa Mbao FC, Metacha Boniphace Mnata anayecheza kwa mkopo kutoka Azam FC, alichaguliwa Mchezaji Bora wa Mechi na kuzawadiwa fedha, dola za Kimarekani 500, zaidi ya Sh. Milioni 1.2 za Tanzania.
  Fainali ya SportPesa Super Cup baina ya timu za Kenya tupu inafanyika hivi sasa Uwanja wa Taifa, Bandari FC ya Mombasa wakimenyana na Kariobangi Sharks.
  Wakenya wamekuwa wakitamba kwenye michuano hiyo tangu ianzishwe, mwaka 2017 Gor Mahia wakiwafunga mahaimu wao, AFC Leopards 3-0 Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam na mwaka jana wakiwafunga Simba SC 2-1 Uwanja wa Afraha mjini Nakuru.
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Deogratias Munishi ‘Dida’, Zana Coulibally, Rashid Juma, Lamine Moro/James Kotei dk46, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Mohammed ‘Mo’ Ibrahim, Hassan Dilunga/Nicholas Gyan dk79, Meddie Kagere/Emmanuel Okwi dk46, Sadney Urikhob na Shiza Kichuya/Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ dk64.
  Mbao FC: Metacha Mnata, Vicent Philipo, Amos Charles, David Mwasa, Erick Mulilo, Ally Kimbo, Said Khamis, Ibrahim Hashim, Raphael Siame, Herbet Lukindo/Peter Mwangosi dk57 na Hamim Abdukarim/Gervas Bernard dk44.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA WAIPIGA MBAO KWA MATUTA NA KUSHIKA NAFASI YA TATU SPORTPRSA CUP Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top