• HABARI MPYA

    Friday, January 11, 2019

    MAHAKAMA YAZUIA UCHAGUZI YANGA BAADA YA WANACHAMA KUFUNGUA KESI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeusitisha uchaguzi mdogo wa Yanga uliopangwa kufanyika Jumapili katika Ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi, Osyterbay mjini Dar es Salaam kwa agizo la Mahakama.
    Akizungumza na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Malangwe Mchungahela amesema kwamba wameamua kuahirisha uchaguzi huo baada ya baadhi ya wanachama wa klabu hiyo kuweka pingamizi mahakamani.
    “Ndugu waandishi ratiba yetu ya uchaguzi wa Yanga ni Jumapili, sasa wakati tupo kwenye kikao tukapata taarifa kuwa kuna baadhi ya wanachama wa Yanga wamefungua kesi za kusimamisha uchaguzi hapa Dar es Salaam,  Mbeya, Dodoma na Morogoro na sehemu nyingine,”amesesema Mchungahela na kuongeza; 

    “Sasa sisi kama Kamati hatutaki kugongana na mhimili wa mahakama, kwa sababu tumesikia kuna sehemu nyingine wameanza kusikiliza mashauri hivyo tumeamua kusimamisha uchaguzi usifanyike Jumapili hadi tupate courty order, maana kesi nyingine zimeanza kusikilizwa leo na Jumatatu tutawaita ili tuwaambie nini kinaendelea,” aliongeza Mchungahela.
    Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF amewataka pia wagombea kusitisha mikutano yao ya kampeni ikiwemo mdahalo uliopangwa kufanyika leo na kurushwa live na Televiasheni ya Azam TV.
    Wagombea watatu wamepitishwa kuwania nafasi ya Uenyekiti ambao ni Dk. Jonas Benedict Tiboroha, Mbaraka Hussein Igangula na Erick Ninga, wakati Yono Kevela, Titus Eliakim Osoro na Salum Magege Chota wanawania Umakamu Mwenyekiti.
    Wagombea wengine 16 wanawania Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ambao ni Hamad Ally Islam, Benjamin Jackson Mwakasonda, Sylvester Haule, Salim Seif, Shafil Amri, Said Kambi, Dominick Francis, Seko Jihadhari, Ally Omar Msigwa, Arafat Ally Hajji, Frank Kalokola, Ramadhani Said, Leonard Marango, Bernard Faustin Mabula, Christopher Kashiririka na Athanas Peter Kazige.
    Uchaguzi huu ni maalum kuziba nafasi za wagombea waliojiuzulu kwa nyakati tofauti baada ya uchaguzi wa Juni 11 mwaka 2016.
    Waliojiuzulu ni aliyekuwa Mwenyekiti Yussuf Manji, Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga na wajumbe wanne, Omary Said Amir, Salum Mkemi, Ayoub Nyenzi na Hashim Abdallah.
    Wajumbe waliobaki katika Kamati ya Utendaji ni wane tu ambao ni Siza Augustino Lymo, Tobias Lingalangala, Samuel Lukumay na Hussein Nyika.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAHAKAMA YAZUIA UCHAGUZI YANGA BAADA YA WANACHAMA KUFUNGUA KESI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top