• HABARI MPYA

  Alhamisi, Januari 31, 2019

  AZAM FC U20 YAWACHAPA VIJANA WENZAO WA YANGA 2-1 CHAMAZI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU ya vijana ya Azam FC chini ya umri wa miaka 20 (Azam U-20) usiku wa jana iliwachapa vijana wenzao wa Yanga mabao 2-1, katika mchezo wa kirafiki uliomalizika Uwanja wa Azam Complex, dar es Salaam.
  Azam U-20 imekuwa na utamaduni wa kucheza mechi mbalimbali za kirafiki ikiwa chini ya Kocha Mkuu wake, Meja Mstaafu Abdul Mingange, lengo likiwa ni kujiweka sawa kwa ajili ya ligi ya vijana na michuano mingine iliyopo mbele yao.
  Mchezo huo ulikuwa ni wa upinzani mkubwa kwa pande zote mbili, jambo ambalo liliwavutia watazamaji waliojitokeza kutazama burudani ya vijana hao, lakini Azam U-20 ikionekana kutawala sehemu kubwa ya kipindi cha pili.
  Vijana wa Azam FC walianza kutangulia dakika ya tatu tu ya mchezo, kwa bao safi la umbali lililofungwa na mshambuliaji wake hatari, Abadi Kawambwa kwa shuti zuri lililomshinda kipa.
  Yanga inayofundishwa na mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Said Maulid ‘SMG’, ilifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika chache baadaye kabla ya kumalizika kwa kipindi cha kwanza kupitia kwa Ramadhan Mrisho, aliyepiga shuti kali la mbali lililomshinda kipa na kufanya timu hizo ziende mapumziko zikiwa nguvu sawa.
  Mshambuliaji Hamisi Ngoengo, aliihakikishia ushindi Azam U-20 kwa bao zuri akimalizia mpira uliotemwa na kipa kufuatia shuti kali lililopigwa na kiungo Novatus Dismas, aliyeonekana kulimiliki eneo la katikati kwa asilimia kubwa akishirikiana na Omary Banda na Emmanuel Kabelege.
  Huku mabeki nao wakifanya kazi kubwa chini ya Lusajo Mwaikenda, beki wa kulia Samweli Onditi aliyekuwa Mchezaji Bora wa mwezi Desemba na kushoto akikamua Abdallah Madirisha, aliyetwaa tuzo ya Mwezi Novemba.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC U20 YAWACHAPA VIJANA WENZAO WA YANGA 2-1 CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top