• HABARI MPYA

    Wednesday, January 16, 2019

    AZAM FC YAAMBULIA SARE KWA RUVU SHOOTING, BIASHARA YASHINDA TENA

    Na Mwandishi Wetu, MLANDIZI
    TIMU ya Ruvu Shooting ya Pwani imetoa sare ya bila kufungana na Azam FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
    Matokeo hayo yanayoiongezea kila timu pointi moja, yanaifanya Azam FC ifikishe pointi 41 baada ya kucheza mechi 18, ikiendelea kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu, nyuma ya Yanga SC yenye pointi 53 za mechi 19 na mbele ya mabingwa watetezi, Simba SC wenye pointi 33 za mechi 14.
    Ruvu Shooting inafikisha pointi 24 baada ya kucheza mechi 22 na kupanda kwa nafasi moja tu kutoka ya 14, sasa ikiwa mbele ya Stand United ya Shinyanga yenye pointi 23 za mechi 22.

    Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, bao pekee la Raphael Siame dakika ya 72 limeipa ushindi wa 1-0 Mbao FC dhidi ya Singida United Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.  
    Nayo Biashara United imeendelea kufanya vyema chini ya kocha mpya, Amri Said ‘Stam’ baada ya kuibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Stand United, bao pekee la Waziri Rashid dakika ya 90 Uwanja wa Karume, Musoma mkoani Mara.
    African Lyon imepata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Kagera Sugar Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam. 
    Mabao ya Lyon, timu ya zamani ya Nahodha wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta anayechezea KRC Genk ya Ubelgiji kwa sasa yamefungwa na Jabir Aziz mawili dakika za 24 na 70 na Said Bakari dakika ya 82, wakati ya Kagera yote yamefungwa na Kassim Hamisi dakika za 36 na 87.
    Nayo Ndanda FC imeutumia vyema Uwanja wa nyumbani, Nangwanda Sijaona mjini Mtwara baada ya kuibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya JKT Tanzania mabao yake yakifungwa na Vitalis Mayanga dakika ya 25 na Emmanuel Memba dakika ya 52, wakati la wageni limefungwa na Abrahman Mussa dakika ya 83. 
    Matokeo hayo hayabadilishi msimamo wa Ligi Kuu kwenye nafasi tatu za mwisho, Tanzania Prisons ikiendelea kuzibeba timu nyingine zote 19 kwa pointi zake 19 za mechi 21, juu yake zikiwepo Biashara United yenye pointi 18 za mechi 21 na African Lyon pointi 19 za mechi 22.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC YAAMBULIA SARE KWA RUVU SHOOTING, BIASHARA YASHINDA TENA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top