• HABARI MPYA

  Jumanne, Januari 15, 2019

  TFF KUTANGAZA MCHAKATO MPYA WA UCHAGUZI YANGA BAADA YA WIKI MOJA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imesema uchaguzi wa klabu ya Yanga utaendelea baada ya wiki moja kufuatia kufikia makubaliano na wanachama wa klabu hiyo waliofungua kesi kuzuia uchaguzi huo uliokuwa ufanyike Jumapili iliyopita kuzifuta kesi hizo.
  Mwenyekiti Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Malangwe Ally Mchungahela amesema leo katika taarifa yake kwamba baada Kamati yake itatangaza ratiba mpya ya kukamilisha uchaguzi mdogo wa Yanga baada ya siku saba kuanzia jana.  
  “Ndugu Wana-habari, Ijumaa iliyopita niliwatangazia kusogezwa mbele kwa muda uchaguzi mdogo wa klabu ya Yanga kufuatia taarifa za wimbi la (tulioamini kuwa wana-Yanga) kufungua kesi sehemu mbalimbali nchini kuzuia uchaguzi huo usifanyike na kwamba baadhi ya Mahakama zilishatoa amri hiyo,”.

  Mwenyekiti Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Malangwe Ally Mchungahela amesema ratiba mpya ya uchaguzi mdogo wa Yanga itatangazwa baada ya wiki moja

  “Kwa kuheshimu mamlaka ya ki-Katiba ya Mahakama nchini na kwamba nchi yetu inaheshimu na kufuata utawala wa sheria, Kamati yangu ya Uchaguzi haikuwa na njia nyingine ya kufanya bali kuusogeza mbele kwa muda uchaguzi wa Klabu ya Yanga uliopangwa ufanyike siku mbili baadaye, yaani Jumapili ya tarehe 13/01/2018,”.  
  “Kwa upande wa pili, Kamati ilijikuta na deni kubwa kwa wana-Yanga, deni la kuelezea kilichojiri, kuelezea msingi wa kesi hizo mahakamani zilizosababisha kusogezwa mbele kwa muda uchaguzi katika klabu yao,”. 
  “Hivyo kuanzia Ijumaa jioni, yaani mara tu baada ya kutangaza kusogezwa mbele kwa muda kwa uchaguzi huo, Kamati ilitumia njia mbalimbali kuwafikia wale wote waliofungua kesi ili kujua msingi wa malalamiko yao na uhalali wao kusimama mahakamani dhidi ya Klabu hiyo ya Yanga kwa mujibu wa Katiba ya Yanga,”.  
  “Tumejiridhisha kuwa malalamiko yote yamejikita kwenye maeneo makuu matatu: (i) mosi, uhalali wa wanachama wenye kadi za zamani, kadi za CRDB na kadi za Benki ya Posta kupiga kura; (ii) pili, kukataliwa majina ya wanachama katika baadhi ya matawi ya Yanga kuingizwa kwenye rejista ya wanachama wa Yanga; na (iii) tatu, sintofahamu ya nafasi ya Mwenyekiti wa Yanga hivyo kusababisha baadhi ya wanachama wenye sifa za uongozi, kuwa na mashaka kujitokeza,”.  
  “Kamati ya Uchaguzi, mbali na kuchambua sifa ya uanachama ya walalamikaji hao (ambapo Kamati imebaini kuwa walalamikaji wote kasoro mmoja, si wanachama hai wa Yanga), imepitia malalamiko yote hayo kwa kina na kuwapelekea ujumbe ufuatao walalamikaji wote kwamba: (i)  uanachama wao Yanga una hitilafu ki-Katiba, hivyo hawakuwa na sifa (locus) kupeleka malamamiko yao popote pale kwa kivuli cha uanachama wa klabu hiyo; (ii) Katiba za Yanga, TFF, CAF na FIFA haziruhusu wanachama wao kupeleka malalamiko mahakamani, hivyo utaratibu huo hauna tija mbali na kuiondolea klabu sifa ya kuheshimu taratibu (compliance); (iii) malalamiko yao yote waliyoainisha yanatatulika kwa taratibu zilizopo ndani ya shirikisho, hivyo hawana budi kuondoa kesi hizo mahakamani mara moja,”.  
  “Napenda kuwataarifu kuwa walalamikaji wote wametuelewa na wamekubali kuondoa kesi zao zote mahakamami na hivyo, kuruhusu Kamati yangu kuwasilisha TFF malalamiko yote tuliyoainisha ili yafanyiwe kazi ndani ya siku 7 kuanzia jana na baada ya hapo Kamati itatangaza ratiba ya kukamilisha uchaguzi mdogo wa Yanga,”.  
  “Naomba vilevile nisisitize kwamba uchaguzi huu ni uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi zilizoachwa wazi. Hivyo viongozi wa Yanga tunaowachagua sasa ni wa kipindi kifupi kilichobaki cha takriban mwaka mmoja, kabla ya mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Yanga kuanza. Nihitimishe taarifa yangu kwa kuwashukuru Watanzania na wana-Yanga wote kwa utulivu na uvumilivu mkubwa mliouonesha baada ya uchaguzi wenu mdogo kusogezwa mbele kwa muda,”. 
  Aidha nawaomba wana-Yanga wote wakiongozwa na Wajumbe wa Baraza la Wadhamini, Sekreterieti na Wajumbe waliobaki wa Kamati ya Utendaji, wasichoke maana tumekaribia mwisho wa zoezi hili lenye afya kwa ustawi na maendeleo ya klabu hii kongwe Afrika ya Mashariki na Kati. Timu bora inategemea uongozi bora unaowajibika kwa wanachama,”amesema Mchungahela katika taarifa yake ya leo. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TFF KUTANGAZA MCHAKATO MPYA WA UCHAGUZI YANGA BAADA YA WIKI MOJA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top