• HABARI MPYA

    Thursday, January 24, 2019

    WAMBURA ASEMA FIFA IMEMFUNGIA KWA TAARIFA POTOFU WALIYOPEWA NA TFF

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MAKAMU wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Richard Wambura amepinga uamuzi wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kumfungia maisha, akisema kwamba bodi hiyo ya soka duniani imemuhukumu kwa taarifa potofu.
    Kupitia kwa Mwanasheria wake, Emmanuel Muga, Wambura amesema kwamba FIFA ilipelekewa taarifa potofu na TFF juu ya mteja wake, hivyo imemuhukumu kimakosa.
    Kamati ya Nidhamu ya FIFA chini ya Mwenyekiti wake, Anin Yeboah wa Ghana imekazia hukumu ya Kamati ya Maadili ya TFF kumfungia maisha Wambura kujihusisha na soka iliyotolewa Aprili 6 mwaka jana. 
    Lakini Muga amesema kwamba watakata rufaa FIFA ndani ya siku 10 walizopewa kuhakikisha wanapata haki hao na hawana shaka mwisho wa misukosuko yao umewadia.

    Ikumbukwe Uamuzi ya Kamati za Maadili za TFF kumfungia Wambura maisha kujihusisha na mchezo huo ulitenguliwa na Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam Novemba 30 mwaka jana.
    Uamuzi huo ulitenguliwa na Jaji, Dk. Benhajji Masoud kufuatia kesi iliyofunguliwa na Wambura kupinga kufungiwa maisha na Kamati za Maadili za TFF.
    Kwa uamuzi huo, Wambura alirejeshwa katika madaraka yake ya Umakamu wa Rais wa TFF na Uenyekiti wa Chama cha Soka Mara (FAM) – lakini uongozi wa TFF chini ya Rais Wallace Karia ukakata rufaa kupinga uamuzi wa mahakama.
    Machi mwaka huu Kamati ya Maadili ya TFF chini ya Mwenyekiti wake, Hamidu Mbwezeleni ilimfungia maisha Wambura kutojihusisha na masuala ya soka kwa kumtuhumu kwa makosa matatu.
    Katika taarifa yake, TFF ilisema kwamba ilichukuwa hatua hiyo kwa mujibu wa kifungu cha 73(1) (c) cha Kanuni za Maadili ya TFF Toleo la 2013. 
    Hiyo ni baada ya kikao chake cha Machi 14, mwaka huu ambacho pamoja na mambo mengine, kilimjadili Wambura aliyefikishwa kwenye Kamati hiyo kwa tuhuma za makosa matatu ya kupokea fedha za TFF malipo yasiyo halali, kugushi  barua na kushusha hadhi ya TFF.
    Wambura alifikishwa kwenye Kamati ya Maadili na Sekretarieti ya TFF iliyodai baada ya Kamati ya Ukaguzi kukutana na kupitia mambo mbalimbali ya ukaguzi na suala hilo la Wambura ilionekana linatakiwa kufika kwenye Kamati ya Maadili.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WAMBURA ASEMA FIFA IMEMFUNGIA KWA TAARIFA POTOFU WALIYOPEWA NA TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top