• HABARI MPYA

  Ijumaa, Januari 25, 2019

  AZAM FC YAPANIA KUWAADHIBU BIASHARA UNITED LEO USIKU CHAMAZI

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC leo inateremka Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Dar es Salaam kuanzia Saa 1:00 usiku kumenyana na Biashara United ya Mara katika mfululizo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
  Azam FC imeonekana kufanya vema kwenye msimu huu wa ligi ikiwa nafasi ya pili kwa pointi 44, na itaingia kumenyana na timu hiyo ikitoka kuichapa Mwadui, kwa bao lililofungwa na mshambuliaji Donald Ngoma, akimalizia kazi nzuri ya kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
  Biashara United iliyonafasi ya 18 kwenye msimamo wa ligi kwa pointi zake 20, imetoka kupoteza mchezo wa mwisho wa ligi ikifungwa na Kagera Sugar mabao 2-1 ugenini katika Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba, Kagera.

  Kikosi hicho kimekuwa kwenye maandalizi makali, kuelekea mchezo huo ambapo itanufaika na urejeo wa mabeki wake wawili, nahodha Aggrey Morris na Nickolas Wadada, waliokosa mechi iliyopita kutokana na wawili hao kila mmoja kukusanya kadi tatu za njano.
  Benchi la ufundi la Azam FC chini ya Kocha Mkuu, Hans Van Der Pluijm pamoja na wachezaji, wanauchukulia kwa uzito mkubwa mtanange huo, wakitaka kuendeleza wimbi la ushindi ili kuendelea na vita ya kuwania taji la ligi hiyo msimu huu.
  Mabingwa hao mara tatu mfululizo wa Kombe la Mapinduzi, ambao pia wamebeba ubingwa mwingine wa Kombe la Kagame kwa mara ya pili mfululizo, wataendelea kukosa hudumu ya mabeki wake David Mwantika, Daniel Amoah, ambao bado ni wagonjwa.
  Aidha pia itawakosa viungo wake, nahodha msaidizi Frank Domayo ‘Chumvi’, Tafadzwa Kutinyu, winga Joseph Kimwaga na mshambuliaji Paul Peter, ambao wanaendelea na programu ya mwisho ya kurejea uwanjani baada ya kupona majeraha yao.
  Hii itakuwa ni mara ya pili kwa timu hizo kukutana kwenye mechi ya ligi, zilipokutana raundi ya kwanza katika mechi ya kwanza kihistoria, zilitoka suluhu, mchezo uliopigwa Uwanja wa Karume, mijini Musoma.
  Hadi sasa kikosi cha Azam FC kimeshacheza jumla ya mechi 18 za ligi, kikishinda mara 12, kikitoa sare tano na kupoteza mara moja dhidi ya Mtibwa Sugar (2-0) ikifungwa ugenini.
  Mara baada ya mchezo dhidi ya Biashara, itahamishia vita yake kubwa kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Pamba, utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Jumatatu ijayo saa 1.00 usiku.    
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC YAPANIA KUWAADHIBU BIASHARA UNITED LEO USIKU CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top