• HABARI MPYA

  Tuesday, January 29, 2019

  MULAMBA ALIYEWEKA REKODI YA MABAO AFCON AFARIKI DUNIA

  MFUNGAJI wa mabao tisa ya rekodi Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, Pierre Ndaye Mulamba amefariki dunia Jumamosi mjini Cape Town akiwa ana umri wa miaka 70, amesema Waziri wa Michezo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  Mulamba aliichezea Zaire (sasa DRC) katika fainali za AFCON za 1974 nchini Misri, ambazo nchi yake ilitwaa taji hilo baada ya kushinda mechi ya marudiano na Zambia.
  Ilikuwa ni mara ya pili na ya mwisho kwa nchi hiyo tajiri ya madini kutwaa taji hilo.
  Kwa mujibu wa taarifa, Mulamba amekuwa akisumbuliwa na maradhi kwa muda na awali alipelekwa India kwa matibabu kabla ya kuhamishiwa Afrika Kusini Agosti mwaka jana kwa matibabu zaidi.
  Pierre Ndaye Mulamba (kushoto) amefariki dunia Jumamosi mjini Cape Town akiwa ana umri wa miaka 70

  Pierre Ndaye Mulamba (wa pili kulia) akiwa na wachezaji wenzake wa DRC enzi zake
  Pierre Ndaye Mulamba enzi za uhai wake akiitumikia timu ya taifa ya Kongo, zamani Zaire

  Waziri wa Michezo wa DRC, Papy Niango amesema katika taarifa yake kwamba Mulamba amefariki dunia mapema asubuhi ya Januari 26.
  Akijulikana kwa jina la utani la Mutumbula, yaani Muuwaji, Mulamba alifunga mabao mawili dhidi ya Guinea na moja dhidi ya Mauritius mwaka 1974 katika mechi za makundi za AFCON.
  Kilichofuatia ni mafanikio ya kukumbukwa, Zaire ikiifunga Misri katika Nusu Fainali 3-2 na Zambia katika fainali 2-0 katika mchezo wa marudio baada ya mechi ya kwanza kumalizika kwa sare ya 2-2, huku Mulamba akifunga mabao sita kwenye mechi hizo.
  Nyota wa Cameroon, Samuel Eto'o anashikilia rekodi ya kufunga mabao mengi jumla kwenye fainali za AFCON, 18.
  Mulamba pia aliisaidia AS Vita kushinda taji la Klabu Bingwa Afrika, sasa Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1973.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MULAMBA ALIYEWEKA REKODI YA MABAO AFCON AFARIKI DUNIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top