• HABARI MPYA

  Jumatatu, Januari 28, 2019

  AZAM FC YATINGA 16 BORA KOMBE LA TFF, MTIBWA NAYO YAITOA MAJI MAJI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU ya Azam FC imefanikiwa kuingia hatua ya 16 Bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), au Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Pamba SC ya Mwanza Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam usiku wa leo. 
  Kwa ushindi huo uliotokana na mabao ya Ramadhani Yahya Singano ‘Messi’ dakika za 18 na 52, Azam FC itakutana na mshindi kati ya Rhino Rangers na Stand United.
  Mechi nyingine za leo, mabingwa watetezi Mtibwa Sugar imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Maji Maji ya Songea Uwanja wa Manungu, Turiani mjini Morogoro na Namungu FC imeibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Mighty Elephant.

  Mtibwa Sugar ambayo mabao yake yamefungwa na mshambuliaji wake chipukizi, Riffat Khamisi dakika ya nne na 59 dhidi ya lile la Maji Maji lililofungwa na Anthony Mwingira dakika ya saba, itakutana na KMC iliyoitoa Pan Africans, wakati Namungo FC sasa itakutana na mshindi kati ya Yanga SC na Biashara United.
  Timu nyingine zilizofuzu hatua ya 16 Bora mbali na KMC iliyoifunga 5-1 Pan Africans Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam ni Kagera Sugar iliyoitoa Mbeya Kwanza kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya 2-2, Mbeya City iliyoitoa Mashujaa FC kwa kuichapa 1-0 mjini Kigoma.
  Nyingine ni Lipuli FC ya Iringa iliyoitoa Polisi Tanzania kwa penalti 3-2 baada ya sare ya 1-1 Uwanja wa Ushirika mjini Moshi, Alliance FC iliyoitoa La Familia kwa kuichapa 2-0 Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza, Dodoma FC iliyoitoa Transit Camp kwa penalti 5-4 kufuatia sare ya 1-1 Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma. 
  Nayo Coastal Union ya Tanga iliwatupa nje Kitayosce kwa kuwachapa mabao 2-0 huko Moshi mkoani Kilimajaro, African Lyon iliyowatoa Friends Rangers kwa penalti 4-2 kufuatia sare ya 0-0 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam na Dar City iliyowatoa Cosmopolitan kwa penalti pia, 4-2 baada ya sare ya 0-0.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC YATINGA 16 BORA KOMBE LA TFF, MTIBWA NAYO YAITOA MAJI MAJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top