• HABARI MPYA

  Jumapili, Januari 20, 2019

  COASTAL, KAGERA SUGAR, JKT, ALLIANCE ZASHINDA NYUMBANI LIGI KUU LEO

  Na Mwandishi Wetu, TANGA
  TIMU ya Coastal Union imetumia vizuri Uwanja wa nyumbani, Mkwakwani mjini Tanga baada ya kuibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya African Lyon mchana wa leo katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
  Ushindi huo uliotokana na mabao ya Andrew Simchimba dakika ya 49 na Issa Abushehe dakika ya 90 na ushei unakujaa baada ya timu hiyo kufungwa 5-2 na KMC katika mchezo wake uliopita mjini Dar es Salaam.
  Matokeo hayo yanaifanya Coastal Union inayofundishwa na mchezaji wake wa zamani, Juma Mgunda ifikishe pointi 28 baada ya kucheza mechi 21, ikipanda kutoka nafasi ya 14 hadi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu yenye timu 20, wakati Lyon inabaki nafasi ya 19 na pointi zake 19 za mechi 23.

  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, JKT Tanzania imeibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Mbao FC ya Mwanza, bao pekee la kujifunga la beki Peter Mwangosi dakika ya nne Uwanja wa Meja Isamuhyo, Mbweni nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
  JKT inafikisha pointi 25 baada ya ushindi huo, kufuatia kucheza mechi 22 na inajiinua kutoka nafasi ya 17 hadi ya 12, wakati Mbao FC inabaki na pointi zake 33 baada ya kucheza mechi 23 ikiendelea kushika nafasi ya sita.
  Nayo Alliance FC imeibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza katika mchezo wa ligi hiyo leo.
  Mabao yote ya Alliance FC inayocheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu huu yamefungwa na Dickson Ambundo dakika ya 33 na 55, wakati la Mbeya City limefungwa na Iddi Suleiman ‘Nado’ dakika ya 81.
  Alliance FC inapanda hadi nafasi ya tisa kutoka ya 14, ikifikisha pointi 28 baada ya kucheza mechi 23, wakati Mbeya City inayobaki na pointi zake 26 baada ya kucheza mechi 21, inateremka tena kwa nafasi moja hadi ya 11.
  Ruvu Shooting imelazimishwa sare ya 0-0 na Tanzania Prisons Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani wakati Kagera Sugar nayo imeibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Biashara United ya Mara Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
  Mabao ya Kagera Sugar inayofundishwa na Nahodha wa zamani wa Tanzania, Mecky Mexime yamefungwa na Kassim Hamisi dakika ya 17 na Omary Mponda dakika ya 70, wakati la Biashara limefungwa na George Makang'a dakika ya 15.
  Ruvu inapanda kwa nafasi moja hadi ya 14, ikifikisha pointi 25 katika mechi 23, Prisons wanafikisha pointi 17 katika mechi ya 22 na wanabaki mkiani, nafasi ya 20, kagera Sugar wanafikisha pointi 28 katika mechi 21 na kupanda kutoka nafasi ya 12 hadi ya nane, wakati Biashara inabaki nafasi ya 18 na pointi zake 20 za mechi 22 sasa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: COASTAL, KAGERA SUGAR, JKT, ALLIANCE ZASHINDA NYUMBANI LIGI KUU LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top