• HABARI MPYA

  Saturday, January 19, 2019

  SAMATTA AFUNGA NA KUTOA PASI YA BAO GENK YASHINDA 3-2 UGENINI UBELGIJI

  Na Mwandishi Wetu, ST. TROND
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta usiku wa jana amefunga na kutoa pasi ya bao, timu yake, KRC Genk ikishinda 3-2 dhidi ya wenyeji, Sint-Truiden katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Sint-Truiden mjini St. Trond.
  Kwa ushindi huo kwenye mchezo wake wa kwanza kabisa mwaka mpya, 2019, Genk inafikisha pointi 51 baada ya kucheza mechi 22, ikiendelea kuongoza ligi hiyo kwa pointi 10 zaidi ya Club Brugge inayofuatia kwenye nafasi ya pili. 
  Samatta aliifungia Genk bao lake dakika ya 29 akimalizia pasi ya mshambuliaji mwenzake, Dieumerci N'Dongala kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  Hilo lilikuwa bao la kusawazisha baada ya Mkongo mwingine, Jordan Rolly Botaka kuanza kuifungia Sint-Truiden dakika ya pili tu na Mfaransa, Yohan Boli akawafungia wenyeji bao la pili dakika ya 70.
  Mbwana Samatta akipongezwa na wenzake usiku wa jana baada ya kufunga 
  Mbwana Samatta akifunga bao lake la kwanza la mwaka moya, 2019 

  Mbwana Samatta akiita pasi mbele ya beki wa Sint-Truiden  jana Uwanja wa Sint-Truiden mjini St. Trond 

  Samatta akaibuka tena baada ya kumsetia mshambuliaji mwenzake, Mbelgiji Leandro Trossard kuifungia bao la kusawazisha Genk dakika ya 75.
  Mkongo N'Dongala akaifungia bao la ushindi Genk dakika ya 80, akimalizia pasi ya Trossard, kabla ya Samatta kumpisha Zinho Gano dakika ya 90 na ushei.
  Samatta mwenye umri wa miaka 26, amefikisha jumla ya mabao 55 katika mechi 138 za mashindano yote alizoichezea KRC Genk tangu amejiunga nayo Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  Kwenye Ligi ya Ubelgiji amefikisha mabao 40 katika mechi 106, wakati Europa League amefunga mabao 14 katika mechi 22 na katika Kombe la Ubelgiji amefunga mabao mawili katika mechi tisa.
  Kikosi cha STVV kilikuwa; Steppe, Garcia, De Sart, De Petter, Botaka, Sankhon, Boli, Asamoah, Kamada, Teixeira and Sekine/Janssens dk85.
  KRC Genk; Jackers, Maehle, Aidoo, Dewaest, Uronen, Berge, Malinovskyi, Pozuelo/Heynen dk85, Ndongala, Trossard and Samatta/Gano dk90+3.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SAMATTA AFUNGA NA KUTOA PASI YA BAO GENK YASHINDA 3-2 UGENINI UBELGIJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top