• HABARI MPYA

  Jumapili, Januari 20, 2019

  JANA IMEPIGWA 5-0, LAKINI SIMBA INAWEZA KUWA BINGWA AFRIKA

  TIMU ya Simba SC jana imepoteza mechi ya kwanza Kundi D Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuchapwa mabao 5-0 na wenyeji, AS Vita Uwanja wa Martyrs de la Pentecote zamani Kamanyola, uliopo eneo la Lingwala mjini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). 
  Kipigo hicho kinakuja baada ya Simba SC kuanza vyema mchezo wake wa kwanza ikishinda 3-0 dhidi ya JS Saoura ya Algeria Jumamosi ya wiki iliyopita mjini Dar es Salaam.
  Mshambuliaji Jean-Marc Makusu Mundele ndiye aliyeanza kuwainua mashabiki wa AS Vita baada ya kufunga bao la kwanza dakika ya 14 akimalizia pasi ya Glody Ngonda Muzinga.

  Beki Botuli Padou Bompunga aliyekuwa anacheza badala ya Dharles Kalonji jana ambaye aliyekuwa anatumikia adhabu ya kadi nyekundu, akaifungia AS Vita bao la pili dakika ya 19 akimalizia kona ya Ngonda. 
  Kiungo Fabrice Luamba Ngoma akaifungia AS Vita bao la tatu kwa penalti dakika ya 45 na ushei akimtungua kipa namba moja wa Tanzania, Aishi Salum Manula kufuatia beki Muivory Coast wa Simba SC, Serge Wawa Pascal kumuangusha mchezaji huyo kwenye boksi.
  Kocha wa Simba SC, Mbelgiji Patrick Aussems na wachezaji wake walimfuata refa, Mahamadou Keita na wasaidizi wake, Seydou Tiama, Sidiki Sidibe pamoja na mwamuzi wa akiba, Abdoulaye Sissoko wote kutoka Mali kuwalalamikia kwa uchezeshaji wao baada ya kipindi cha kwanza.
  Hata hivyo, Keita alikuwa mkali na kuwafukuza Aussems na wachezaji wake huku akionekana kama kuwatishia kuwaadhibu, nao wakaepusha shari kwa kuondoka zao kwenda kujipanga kwa kipindi cha pili.
  Aussems alikianza kipindi cha pili kwa mabadiliko katika safu ya kiungo, akimtoa Muzamil Yassin na kumuingiza Mnyarwanda, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima kabla ya baadaye kumtoa pia Mzambia, Clatous Chama na kumuingiza mzawa, Hassan Dilunga. 
  Lakini mabadiliko hayo hayakuwa na msaada kwa Simba SC, kwani jahazi lake lilizidi kuzama ikipachikwa mabao mawili zaidi.
  Beki Makwekwe Kupa alifunga bao la nne kwa kichwa dakika ya 71 akimalizia kona nzuri iliyochongwa na Tuisila Kisinda, kabla ya Makusu kuwachambua mabeki wa Simba na kipa wao, Manula kuifungia Vita bao la tano dakika ya 74 kufuatia pasi nzuri ya Kazadi Kasengu.
  Baada ya mchezo Aussems aliwafuata tena marefa, ingawa safari hiyo alionekana kama kuwashukuru na kuwapa ‘maneno ya busara’.
  Kikosi cha Simba SC kimerejea leo Dar es Salaam kucheza michuano ya SportPesa Super Cup kabla ya kusafiri kwenda Misri kukamilisha mechi zake za mzunguko wa kwanza Kundi D Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kumenyana na wenyeji, Al Ahly Februari 2.
  Sasa Al Ahly inaongoza Kundi D kwa pointi zake nne, ikifuatiwa AS Vita yenye pointi tatu sawa na Simba huku JS Saoura ikishika mkia kwa pointi yake moja.  
  Baada ya mechi mbili za mwanzo za Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu nimekumbuka juu ya ushiriki wa klabu hiyo kwenye hatua hiyo ya makundi kwa mara ya kwanza mwaka 2003.  
  Mwaka huo, Simba SC ilipangwa Kundi A pamoja na Enyimba ya Nigeria, Ismailia ya Misri na Asec Mimosa ya Ivory Coast.
  Ni kipindi ambacho hatua ya makundi ilihusisha timu nane tu zilizogawanywa katika makundi mawili, tofauti na sasa hatua ya makundi inahusisha timu 16 katika makundi manne na robo fainali inachezwa kwa mtoano.
  Simba ikiwa chini ya kocha Mkenya, James Aggrey Siang’a (sasa marehemu) ilianzia ugenini mjini Aba kwa Enyimba International FC na ikachapwa 3-0 Agosti 10, mwaka 2003. 
  Mechi zilizofuata Agosti 24, mwaka huo Simba SC ikarejea nyumbani na kupata ushindi wa 1-0 dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast.
  Lakini siku mbili kabla, Agosti 22, mwaka huo, Enyimba walikuwa Misri kumenyana na wenyeji, Ismailia na wakachapwa mabao 6-1.
  Kilikuwa kipigo kikali cha kukatisha tamaa, wakitoka kuanza vizuri kwa ushindi wa 3-0 nyumbani dhidi ya Simba – lakini Enyimba wakamalizia vyema mechi yao mzunguko wa kwanza kwa kuichapa 3-1 ASEC Septemba 7 mjini Aba, siku ambayo Simba SC ililazimishwa sare ya 0-0 na Ismailia Uwanja wa Taifa, sasa Uhuru mjini Dar es Salaam.
  Mzunguko wa pili, Enyimba walianzia ugenini wakashinda 2-0 dhidi ya ASEC Septemba 21, siku mbili baada ya Ismailia kuifunga Simba 2-1 Misri.
  Oktoba 5, Enyimba ikachapwa 2-1 na Simba SC kwenye mchezo wa marudiano Dar es Salaam, siku mbili baada ya Ismailia kuipiga 2-0 ASEC Mimosas.
  Mechi za mwisho zilichezwa siku moja, Oktoba 19, 2003, ASEC Mimosas wakaifunga 4-3 Simba SC mjini Abidjan na Enyimba wakaifunga Ismailia 4-2 mjini Aba.
  Enyimba ikamaliza kileleni mwa Kundi A ikikusanya pointi 12, ikifuatiwa na Ismailia iliyokusanya pointi 11, Simba SC pointi saba na ASEC Mimosas pointi nne.
  Enyimba na Ismailia zikatinga Nusu Fainali, Simba SC na ASEC Mimosas zikirejea kwenye mashindano ya nchini mwao baada ya kutolewa.
  Katika Nusu Fainali, Enyimba wakaitoa USM Alger ya Algeria kwa jumla ya mabao 3-2, wakitoa sare ya 1-1 ugenini na kushinda 2-1 mjini Aba, wakati Ismailia ikaitoa Esperance ya Tunisia kwa jumla ya mabao 6-2, wakishinda 3-1 nyumbani na ugenini.
  Fainali ya Ligi ya Mabingwa wa bara hili ikazikutanisha timu za Kundi A tupu na Enyimba wakaibuka mabingwa wa Afrika mwaka 2003 kwa ushindi wa jumla wa 2-1, wakishinda 2-0 nyumbani Aba na kufungwa 1-0 ugenini, Cairo nchini Misri.
  Kipigo cha 6-1 Agosti 22, mwaka 3003 kwa Enyimba nchini Misri mbele ya wenyeji, Ismailia hakikuwavunja nguvu. Hawakujiona hawajui. Walijichukulia waliokosea, wakaenda kufanyia kazi makosa yao na baada ya hapo wakafanya vizuri hadi kuwa mabingwa.
  Ni sawa na Simba tu, kipigo cha jana Kinshasa kimezua maneno mengi, wachezaji wanabezwa, timu inabezwa na mashabiki ndiyo wamekuwa wanyonge kabisa, hususan mbele ya watani wao, Yanga.
  Woga umeingia kwenye timu na wanaona kuna vipigo vya aina hiyo kwenye mechi zijazo pia dhidi ya Al Ahly hata na JS Saoura.
  Hakuna sababu ya wachezaji wa Simba kujiona wanyonge kwa kipigo cha jana. Wajihesabu wamepoteza mechi ya kwanza wakitoka kushinda nyumbani na wajipange kuelekea mechi zijazo, wakifanyia kazi makosa yao.
  Aishi Manula jana karuhusu mabao matano, lakini Vincent Enyiama akiwa langoni mwa Enyimba Agosti 22 aliruhusu mabao sita na baadaye akaja kuwa kipa mkubwa Afrika akicheza klabu za Hapoel Tel Avivya ya Israel na Lille ya Ufaransa. 
  Amekuwa kipa wa kwanza wa Nigeria ‘Super Eagles’ kwa muda mrefu na kushinda taji la Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2003. Aishi anapaswa kujitazama kwenye kioo cha Enyeama na kusimama imara tena kuendelea na kazi yake kama ilivyo kwa wachezaji wote wa Simba SC.
  Simba SC imepoteza mechi, haijapoteza ubora wake ulioifikisha hatua hii – wanachotakiwa kufanya kwa sasa ni kusahihisha makosa yao na kuelekeza nguvu katika mchezo ujao, inawezakana hawa ndiyo mabingwa wapya wa Afrika mwaka huu. Kwani Enyimba ilikuwaje 2003?
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: JANA IMEPIGWA 5-0, LAKINI SIMBA INAWEZA KUWA BINGWA AFRIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top