• HABARI MPYA

    Friday, August 21, 2015

    SAUTI ZA BUSARA 2016 HALITAFANYIKA, TATIZO FEDHA

    TAMASHA la muziki Zanzibar, Sauti za Busara halitafanyika mwakani, 2016 kutokana na uhaba wa fedha, Busara Promotions imethibitisha.
    Taarifa ya Busara Promotions imesema wanasikitika kutangaza kuwa tamasha la Sauti za Busara mwaka 2016 halitakuwepo, hiyo ikiwa ni mara ya kwanza ndani ya miaka 13 Zanzibar kulikosa tamasha hilo la kimataifa, ambalo hufanyika kila wiki ya pili ya mwezi Februari.
    Mkurugenzi Mtendaji wa Busara Promotions, Yusuf Mahmoud (pichani juu), amesema leo; "Uamuzi huu haukuchukuliwa kwa wepesi. Kawaida huwa tunatangaza tarehe za tamasha mwaka mmoja kabla. Lakini baada ya kufanya tamasha lililopita kwa mafanikio, tumekuwa katika hali ya ukosefu wa fedha kwa toleo lijalo la 2016,". 
    "Tulijiwekea  malengo ya kukusanya dola za kimarekani  200,000 kabla ya Julai, wakati tulipokuwa na matumaini ya kutangaza tarehe za Sauti za Busara 2016. Baada ya mikutano mingi na wadau, tulisogeza muda wetu wa kutafuta fedha hadi usiku wa Agosti 19,". 
    "Kiasi ambacho tuna uhakika wa kukipata kuandaa tamasha lijayo kwa sasa kinasimamia kwenye dola za kimarekani 42,000, hivyo basi bado tuna safari ndefu mbele yetu. Kawaida wakati kama huu, tunakuwa tumeshafika mbali kwenye makubaliano ya mikataba mbalimbali kama ya kukodi ukumbi, ukodishaji wa vifaa, wasanii na mameneja, tunaanza kupanga ratiba, maandalizi ya usafiri na malazi kwa wasanii mapema iwezekanavyo,". 
    "Shinikizo zaidi, tumekuwa tukipokea maswali kutoka kwa watu mbalimbali duniani kote wakitaka kujua tarehe za tamasha ili waweze kufanya mipango yao ya safari. Mauzo ya tiketi za Sauti za Busara haijawahi kuwa tatizo, lakini hii inasaidia kulipa 30% ya gharama za tamasha," amesema Yusuf Mahmoud.
    Yusuf amesema matamasha yanahamasisha vijana kupenda utamaduni wao, kutoa fursa kwa wasanii na wataalamu wa muziki kukutana na kujifunza, yanashawishi uhai wa tamaduni, pia yanatoa nafasi za ajira kwa watu wa ndani na kutoa mifano ya utalii ambayo inathamini na kuheshimu utamaduni wa ndani. 
    Hata hivyo, wamekuwa wakifanya tamasha hilo tangu mwaka 2004 bila msaada wowote wa kifedha kutoka serikali ya Zanzibar, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au Jumuiya ya Afrika Mashariki. 
    Amesema pamoja na jitihada nyingi, msaada kutoka kwa wahisani, balozi na wafanyabiashara unazidi kupungua siku hadi siku wakati Busara Promotions ni shirika lisilo la kiserikali na tamasha haliko kibiashara. 
    "Wengine walipendekeza tujaribu kuomba pesa kupitia mitandao. Hata hivyo, kwa kweli ili kuwa endelevu zaidi, kipaumbele chetu kabla ya toleo la 2017  kitakuwa ni kuendeleza ushirikiano wa muda mrefu na wadhamini na wafadhili ambao wanakubaliana na  mtazamo wetu," amesema. 
    Katika kipindi cha miaka 12 iliyopita, Busara imewavutia maelfu ya wageni kutoka kila pembe ya dunia  kuja Zanzibar, wakati ambayo hakuwa msimu wa wageni wengi. Ndege zote zinazokuja Zanzibar kipindi cha tamasha zinajaa, hoteli na migahawa vinajaa, maduka yaliyopo maeneo ya Mji Mkongwe yanapata wateja wengi zaidi. 
    Hata makadirio yanaonyesha tangu mwaka 2004 tamasha limekiingizia kisiwa mapato ya kiasi dola za kimarekami milioni 70 na Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC imeliweka Sauti za Busara kama moja ya matamasha ya muziki bora na ya kuheshimika zaidi Afrika, huku CNN ikiliingiza katika matamasha saba ya muziki ya kiafrika unayotakiwa kuyaona, huku kwenye orodha ya AfroTourism ya linaongoza katika Matamasha bora ya Muziki.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAUTI ZA BUSARA 2016 HALITAFANYIKA, TATIZO FEDHA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top