• HABARI MPYA

  Jumanne, Agosti 25, 2015

  AISHI MANULA ATEMWA STARS KAMBI YA UTURUKI, TIMU KUCHEZA NA LIBYA IJUMAA

  KIPA anayeonekana kuwa bora zaidi kwa sasa, Aishi Manula (pichani kushoto) wa Azam FC ameachwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kilichopo kambini Uturuki. 
  Taarifa ya Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto, imesema kwamba Aishi Manula hakuweza kusafiri na timu kutokana na kuwa majeruhi baada ya kuumia katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga SC Jumamosi.
  Yanga SC ilishinda kwa penalti 8-7 mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya sare ya 0-0 na Aishi alimaliza mechi yote.
  Wachezaji 21 wapo kambini Uturuki chini ya kocha Mkuu Charles Boniface Mkwasa, Msaidizi wake, Hemed Morocco, kocha wa makipa Manyika Peter na Mshauri wa Ufundi, Abdallah Kibadeni.
  Wachezaji wa Taifa Stars wakifanya mazoezi leo mjini Kartepe, Uturuki

  Hao ni makipa Ally Mustafa ‘Barthez’, Said Mohamed, mabeki Juma Abdul, Shomari Kapombe, Mwinyi Haji Mngwali, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka, Abdi Banda, Kelvin Yondani na Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
  Viungo ni Frank Domayo, Himid Mao, Mudathir Yahya, Salum Telela, Said Ndemla na washambuliaji ni Simon Msuva, Deus Kaseke, John Bocco, Rashid Mandawa, Farid Musa na Ibrahim Hajibu. 
  Stars inatarajiwa kucheza mchezo wa kirafiki na Libya usiku wa ijumaa kwenye moja ya viwanja vilivyopo hoteli ya Green Park mjini Kartepe, Uturuki.
  Taifa Stars na Libya zote zimeweka kambi katika hoteli hiyo kujiandaa na mechi za kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika na usiku wa Ijumaa zitamenyana katika mchezo wa kirafiki.
  Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa anatarajiwa kuutumia mchezo huo kukipima kikosi chake kwa mara ya kwanza humo, baada ya mazoezi ya siku nne.
  Mkwasa amesema huduma na vifaa vilivyopo katika hoteli waliyofikia (viwanja, gym) wanavyotumia kwa ajili ya mazoezi ni vizuri, hivyo ratiba yake ya mazoezi inakwenda kama alivyopanga katika maandalizi ya wiki moja ya kuajiandaa na mchezo dhidi ya Nigeria.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AISHI MANULA ATEMWA STARS KAMBI YA UTURUKI, TIMU KUCHEZA NA LIBYA IJUMAA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top