• HABARI MPYA

  Alhamisi, Agosti 20, 2015

  SIMBA SC YASHINDWA BEI YA NDAYISENGA, AKWEA ‘PIPA’ KUREJEA BURUNDI, DOGO LAKE NIANG KUTUA ALFAJIRI KUCHUKUA NAFASI

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI Mrundi, Kevin Ndayisenga amesitisha mpango wa kujiunga na Simba SC na kuamua kurejea kwao- huku kukiwa na habari  Msenegali Papa Niang atatua Alfajiri ya kesho kuchukua nafasi.
  Ndayisenga anaondoka usiku huu baada ya Simba SC kushindwa kufika gharama za manunuzi ya mchezaji huyo.
  Habari ambazo BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE imezipata kutoka Simba SC ni kwamba mchezaji alikuwa tayari kubaki, lakini wakala wake akakwamisha dili kwa dau kubwa alilotaja.
  Kevin Ndayisenga anaondoka Simba SC baada ya kuvutia katika mchezo dhidi ya URA akifunga bao zuri na kuwasisimua mashabiki wa timu hiyo

  Simba SC ilitarajia kumsajili mchezaji huyo kwa gharama zisizozidi dola 30,000 jumla pamoja na malipo ya klabu yake- kwa maana hiyo imeamua kuachana naye.
  Habari za kuondoka kwa Ndayisenga zitawashitua mno wana Simba SC, kwani mchezaji huyo alicheza vizuri mchezo wa kirafiki dhidi ya URA mwishoni mwa wiki na kufunga bao.
  Kiwango chake katika mchezo huo Simba SC ilishinda 2-1 kiliwasisimua mashabiki wa timu hiyo ya Msimbazi na kuanza kutamba wamepata ‘kifaa’ cha kuwaadabisha wapinzani- hivyo kuondoka kwake kutawasononesha dhahiri.
  Ikumbukwe, Ndayisenga alikuwa mpango mbadala baada ya Simba SC kumkosa mshambuliaji mwingine hatari wa Vital’O, Laudit Mavugo kufuatia klabu mbili za nchini humo kupandisha thamani ya mchezaji huyo na kuwa Sh. Milioni 200, badala 110 zilizokubaliwa awali.
  Aidha, kuibuka pia kwa mzozo mpya kati ya klabu ya Vital’O FC na Solidarity FC, inayodai kumlea Mavugo na kudai ina hakimiliki ya mchezaji huyo nako kuliishitua Simba.
  Vital’O ikaikoroga zaidi Simba SC baada ya kudai kiwepo kipengele cha wao kupata asilimia 50 kama mchezaji huyo atauzwa na Wekundu hao wa Msimbazi kwenda klabu nyingine.   
  Simba SC ilisema inaleta mshambuliaji mwingine, Makan Dembele kutoka Mali na kipa Mreno mwenye asili ya Brazil, Ricardo Ribeiro de Andrade baada ya kumkosa Mavugo.
  Lakini hadi sasa, si mlinda mlango huyo mkongwe wa umri wa miaka 39 wala Dembele anayetokea JS Kabylie ya Algeria aliyeonekana nchini kwa zaidi ya wiki sasa.
  Papa Niang kushoto akifanya yake wakati anacheza FC Jaro ya Finland

  Papa Niang anatarajiwa kuwasili Alfajiri ya kesho Dar es Salaam

  Na sasa baada ya Ndayisenga kuondoka, Simba SC wanasema anakuja mshambuliaji mwingine, Papa Niang anayechezea klabu ya Alianza F.C. ya El Salvador ambaye ni mdogo wa mshambuliaji wa kimataifa wa zamani wa Senegal, Mamadou Niang.
  Mchezaji huyo aliyewahi kuchezea timu za CF Mounana ya Gabon, Al Shabab SC ya Kuwait, FC Vostok ya Kazakhstan, FF Jaro, AC Oulu na FC OPA za Finland, ni mdogo wa damu wa Niang ambaye kwa sasa anamalizia soka yake FF Jaro baada ya kuwika Ulaya na Asia. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC YASHINDWA BEI YA NDAYISENGA, AKWEA ‘PIPA’ KUREJEA BURUNDI, DOGO LAKE NIANG KUTUA ALFAJIRI KUCHUKUA NAFASI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top