• HABARI MPYA

  Ijumaa, Agosti 21, 2015

  DOGO LAKE NIANG LATUA SIMBA SC NA KUSEMA; “KUFUNGA MABAO NDIYO KITU NACHOPENDA”

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI Msenegali, Papa Niang amewasili asubuhi ya leo kwa ajili ya majaribio ya kujiunga na Simba SC na kusema kwamba; “Kufunga mabao ni kitu nachopenda”.
  Mchezaji huyo kutoka klabu ya Alianza F.C. ya El Salvador ambaye ni mdogo wa mshambuliaji wa kimataifa wa zamani wa Senegal, Mamadou Niang, amesema kwamba yuko tayari kwa majaribio kwa sababu anajiamini yuko fiti.
  “Mimi ni mchezaji ambaye niko tayari kucheza, na ninajua. Ninajiamini, hata sasa nakwenda uwanjani nafanya kazi. Naamini mambo yatakwenda vizuri,”alisema Niang akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE baada ya kutua nchini.
  Mchezaji huyo aliyewahi kuchezea timu za CF Mounana ya Gabon, Al Shabab SC ya Kuwait, FC Vostok ya Kazakhstan, FF Jaro, AC Oulu na FC OPA za Finland amesema kwamba kufunga mabao ndiyo kitu anachopenda.
  “Kufunga mabao, nafunga sana, na ni kitu nachopenda kufunga na kushangilia mabao, kama kaka yangu (Mamadou),”amesema mdogo huyo wa damu wa Mamadou Niang ambaye kwa sasa anamalizia soka yake FF Jaro baada ya kuwika Ulaya na Asia. 
  Papa Niang baada ya kuwasili Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam leo

  Simba SC imemleta mpachika mabao huyo, baada ya kushindwana na Mrundi, Kevin Ndayisenga aliyerejea kwao jana usiku baada ya Simba SC kushindwa kufika gharama za manunuzi yake.
  Habari za kuondoka kwa Ndayisenga zimewashitua mno wana Simba SC, kwani mchezaji huyo alicheza vizuri mchezo wa kirafiki dhidi ya URA mwishoni mwa wiki na kufunga bao.
  Kiwango chake katika mchezo huo Simba SC ilishinda 2-1 kiliwasisimua mashabiki wa timu hiyo ya Msimbazi na kuanza kutamba wamepata ‘kifaa’ cha kuwaadabisha wapinzani.
  Ikumbukwe, Ndayisenga alikuwa mpango mbadala baada ya Simba SC kumkosa mshambuliaji mwingine hatari wa Vital’O, Laudit Mavugo kufuatia klabu mbili za nchini humo kupandisha thamani ya mchezaji huyo na kuwa Sh. Milioni 200, badala 110 zilizokubaliwa awali.
  Aidha, kuibuka pia kwa mzozo mpya kati ya klabu ya Vital’O FC na Solidarity FC, inayodai kumlea Mavugo na kudai ina hakimiliki ya mchezaji huyo nako kuliishitua Simba.
  Vital’O ikaikoroga zaidi Simba SC baada ya kudai kiwepo kipengele cha wao kupata asilimia 50 kama mchezaji huyo atauzwa na Wekundu hao wa Msimbazi kwenda klabu nyingine.
  Niang alionekana mwenye kujiamini baada ya kuwasili Dar es Salaam
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: DOGO LAKE NIANG LATUA SIMBA SC NA KUSEMA; “KUFUNGA MABAO NDIYO KITU NACHOPENDA” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top