• HABARI MPYA

  Jumatano, Agosti 26, 2015

  HAKUNA WA KUIZUIA YANGA KUTETEA UBINGWA, ATAMBA MKALI WA MABAO MALIMI BUSUNGU

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI mpya wa Yanga SC, Malimi Busungu amesema kwamba wana kikosi kizuri ambacho kitatetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana mjini Dar es Salaam, Busungu amesema kwamba Yanga SC bado ni timu bora zaidi kwa sasa Tanzania na ubingwa ni wao tena.
  “Tuko vizuri kama timu na wachezaji mmoja mmoja wote wapo vizuri pia, kuna morali, umoja na mshikamano ndani ya timu, sote lengo letu ni moja, matokeo mazuri kwa ajili ya timu,”amesema.
  Malimi Busungu (kulia) akifurahia na mchezaji mwenzake, Deus Kaseke baada ya mechi ya Ngao mwishoni mwa wiki iliyopita

  Busungu ambaye alikuwa benchi muda wote wakati Yanga SC inatwaa Ngao ya Jamii kwa kuifunga Azam FC kwa penalti 8-7 Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salam baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika 90, amesema kwamba ubora wao wataudhihirisha zaidi ligi itakapoanza.
  “Watu wataona Ligi itakapoanza, sidhani kama itatokea timu ya kutusumbua. Ugumu utakuwepo kwa sababu hii ni ligi, lakini utakuwa ugumu wa kawaida sana,”amesema.
  Busungu amesema kwamba wachezaji wengi waliopo Yanga SC wana uzoefu na Ligi Kuu kwa maana ya kucheza katika viwanja tofauti, vikiwemo vile ambavyo watu wanasema vibovu.
  “Sisi hatuna Uwanja ambao eti utatusumbua, tunaweza kucheza katika mazingira yoyote na tukashinda bila wasiwasi, asiyeamini asubiri ligi ianze,”amesema.
  Busungu amesajiliwa Yanga SC Juni mwaka huu kutoka Mgambo JKT ya Tanga na hadi sasa katika mechi 11 alizocheza timu ya Jangwani, amefunga mabao sita.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: HAKUNA WA KUIZUIA YANGA KUTETEA UBINGWA, ATAMBA MKALI WA MABAO MALIMI BUSUNGU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top