• HABARI MPYA

    Sunday, August 30, 2015

    STARS YA BAADAYE SARE TENA MOROGORO, KOCHA SHIME APATA MSIBA, AIACHA TIMU

    Na Prince Akbar, MOROGORO
    KOCHA wa timu taifa ya vijana chini ya umri wa 15, Bakari Shime hakuwepo leo asubuhi kwenye benchi wakati timu hiyo inalazimishwa sare ya bila kufungana na Moro Kids katika mchezo wa kirafiki, Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
    Shime hakuwepo kwa sababu amefiwa na kaka yake na kulazimika kusafiri mapema asubuhi ya leo kurejea Dar es Salaam kwa shughuli za mazishi na Meneja, Jemadari Said ambaye pia kitaaluma ni kocha aliiongoza timu.
    Hiyo ni sare ya pili mfululizo baada ya jana pia timu hizo kufungana bao 1-1 jioni Uwanja huo huo wa Jamhuri.
    Akizungumza baada ya mechi, mshambuliaji wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Jemadari Said alisema kwamba sare hizo zimesababishwa na timu hiyo kuwakosa wachezaji watano na tegemeo wa kikosi cha kwanza walioondoka nchini jana kwenda Afrika Kusini. 
    Wachezaji wa U15 wakisalimiana na wa Moro Kids kabla ya mchezo 

    Rais wa TFF, Jamal Malinzi amewapatia nafasi za kufanya majaribio Orlando Pirates ya Afrika Kusini wachezaji watano wa U-15, Asaad Ali Juma wa Zanzibar, Maziku Aman, Issa Abdi wa Dodoma, Kelvin Deogratias wa Geita na Athumani Maulid wa Kigoma.
    Malinzi alipata nafasi hiyo baada ya mazungumzo na Rais wa klabu hiyo, Irvin Khoza ambaye ameahidi iwapo watafuzu watajiunga na timu ya vijana ya Orlando Pirates kuendeleza vipaji vyao.
    Timu hiyo inaandaliwa kwa ajili kucheza mechi za kufuzu Fainali za Vijana Afrika chini ya umri wa miaka 17 mwaka 2017 na kila wiki ya mwisho wa mwezi wamekuwa wakikutana kwa mazoezi na michezo ya kujipima nguvu.
    Hii ni mara ya kwanza timu hiyo kucheza mechi bila kushinda tangu waanze programu hiyo Juni mwaka huu, wakishinda mechi zote zao Mbeya na Julai visiwani Zanzibar. 
    Baada ya mchezo wa leo, wachezaji hao wamerejea Dar es Salaam na kutawanyika- na wanatarajiwa kukutana tena mwishoni mwa Septemba kwa kambi nyingine ya michezo ya kujipima. 
    Kocha Bakari Shime (kushoto) hakuwepo leo kutokana na msiba wa kaka yake
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: STARS YA BAADAYE SARE TENA MOROGORO, KOCHA SHIME APATA MSIBA, AIACHA TIMU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top