• HABARI MPYA

    Monday, August 31, 2015

    SIMBA SC YAFUNGA USAJILI NA NGONGOTI LA SENEGAL

    Na Princess Asia, ZANZIBAR
    MSHAMBULIAJI Msenegali, Pape Aboulaye N’daw amekamilisha idadi ya wachezaji saba wa kigeni Simba SC baada ya kusaini Mkataba jana kufuatia kufuzu majaribio.
    N’daw aliyejaribiwa katika michezo miwili ya kirafiki dhidi ya JKU Simba ikilala 2-0 Jumamosi na Mafunzo, Wekundu wa Msimbazi wakishinda 3-1 jana, amempiku Makan Dembele kutoka Mali ambaye alitaka kusajiliwa bila majaribio.
    Na sasa mchezaji huyo wa zamani wa Dinamo Bucuresti ya Romania anaungana na kipa Vincent Angban kutoka Ivory Coast, mabeki Emery Nimubona wa Burundi, Juuko Murushid, washambuliaji Simon Sserunkuma, Hamisi Kiiza wote wa Uganda na kiungo Justuce Majabvi wa Zimbabwe.
    Pape Aboulaye N'daw amekamilisha idadi ya wachezaji saba wa kigeni Simba SC

    Dirisha la usajili Tanzania limefungwa Saa 6:00 usiku jana na Simba SC imefanikiwa kuwasilisha orodha ya wachezaji wake ndani ya muda.
    Dembele alitua mwishoni mwa wiki Dar es Salaam na alitakiwa kuwasili Zanzibar tangu juzi, lakini akachelewa na baada ya kufika akasema hawezi kufanya majaribio anataka ‘apewe chake’ asaini Mkataba aanze kazi.
    Wakala wake, Mganda Gibby Kalule alikuwa naye mchezaji huyo jukwaani Uwanja wa Amaan, Zanzibar jioni ya jana wakati Simba SC ikicheza mchezo wa kirafiki na Mafunzo na kushinda 3-1.
    Benchi la Ufundi la Simba SC chini ya kocha Mkuu, Muingereza Dylan Kerr amekataa kucheza ‘kamari’ kwa mshambuliaji huyo wa zamani wa JS Kabyle ya Algeria na kuamua kumchukua N’daw ambaye amemuona mazoezini na katika mechi mbili.
    N’daw anaonekana wazi ni mchezaji ambaye akipewa muda anaweza kuja kuisaidia Simba SC kwa baadaye, kwani ni kijana mdogo, mrefu na anacheza kwa akili sana, kinachomkwamisha tu ni kutoelewana na wenzake uwanjani.
    Anaonekana ni mzuri kwa mipira ya juu si tu kwenye lango la adui hata kusaidia ulinzi mipira ya aina hiyo inapoelekezwa kwenye kango la timu yake.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YAFUNGA USAJILI NA NGONGOTI LA SENEGAL Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top