• HABARI MPYA

    Friday, August 21, 2015

    AZAM FC KUMKOSA KIPRE MECHI NA YANGA SC KESHO TAIFA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    AZAM FC itamkosa kiungo wake raia wa Ivory Coast, Kipre Michael Balou katika mchezo wa kesho wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga SC, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Bolou anasumbuliwa na maumivu ya kisigino cha mguu na hajaonekana uwanjani tangu kumalizika kwa msimu uliopita. 
    Lakini tayari kocha Muingereza wa Azam FC, Stewart John Hall amekwishayazoea maisha bila Balou, kwani timu yake ilitwaa Kombe la Kagame mapema mwezi huu bila rasta huyo.
    Kiungo mpya kutoka Rwanda, Jean Baptiste Mugiraneza aliyeziba pengo la Balou wakati wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati anatarajiwa kuendelea na majukumu hayo kesho.
    Kipre Balou (kulia) akiwa na nduguye, Kipre Tchetche (kushoto)

    Mchezo huo unatarajiwa kuanza Saa 10:00 jioni kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na hakutarajiwi kuwa na mabadiliko makubwa kutoka vikosi vilivyokutana mara ya mwisho katika Robo Fainali ya Kombe la Kagame Julai 29, mwaka huu Azam FC ikishinda kwa penalti 5-3 baada ya sare ya 0-0.
    Ingizo jipya upande wa Yanga SC wanatarajiwa kuwa beki Mtogo, Vincent Bossou, kiungo Mzimbabwe Thabani Kamusoko na mshambuliaji Matheo Simon ambao walisajiliwa baada ya Kagame. 
    Upande wa Azam FC itaendelea kumkosa mshambuliaji mpya, Mkenya Alan Wanga iliyemsajili Julai kutoka El Merreikh ya Sudan, ambaye amechelewa kuungana na wenzake kutokana na msiba wa mama yake mzazi.
    Brian Majwega pia anatarajiwa kuendelea kukosekana, lakini Ramadhani Singano ‘Messi’ yuko fiti na kuhusu kuanza mbele ya Farid Mussa aliyeng’ara Kombe la Kagame, Stewart ataamua. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC KUMKOSA KIPRE MECHI NA YANGA SC KESHO TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top