• HABARI MPYA

  Alhamisi, Agosti 20, 2015

  NKONGO ‘APIGWA CHINI’ YANGA NA AZAM, SASA MARTIN SAANYA KUKIPULIZA JUMAMOSI TAIFA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limemteua mwamuzi wa kati Martin Saanya kuchezesha mchezo wa Ngao ya Jamii Jumamosi kati ya Yanga SC na Azam FC Uwanja wa Taifa, Dar se Salaam.
  Saanya anachukua nafasi ya Israle Nkongo aliyekua amepangwa awali, lakini ameshindwa kazi hiyo kutokana na kusumbuliwa na misuli ya paja.
  Taarifa ya TFF imesema kwamba, Nkongo atakuwa nje ya Uwanja kwa takribani wiki mbili akijiuguza na ndiyo maana TFF imelazimika kubadilisha mwamuzi. Pamoja na hayo, Nkongo ni refa ambaye Yanga hawana imani tangu mwaka 2012.

  Wachezaji wa Yanga SC wakimkimbiza Nkongo Machi 10, mwaka 2012 Uwanja wa Taifa

  Nkongo aliwahi kupigwa na wachezaji wa Yanga SC Machi 10, 2012 timu hiyo ikifungwa 3-1 na Azam FC katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kumtoa kwa kadi nyekundu beki Nadir Haroub 'Cannavaro' akiwa tayari ametoa kadi nyekundu kwa kiungo Haruna Niyonzima pia. 
  Stefano Mwasyika aliyehamia Ruvu Shooting alimtupia ngumi ya ‘kibondia’ Nkongo na Nadir Haroub ‘Canavaro’ alionekana kuhusika katika vurugu hizo wote wakafungiwa na TFF, enzi hizo Rais ni Leodegar Tenga. 
  Mashabiki wa Yanga SC walifanya vurugu kubwa na kuvunja viti Uwanja wa Taifa siku hiyo.

  Refa Martin Saanya (wa pili kushoto) akimdhibiti aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga, Didier Kavumbangu asipigane na beki wa Simba SC, aliyekuwa Nassor Masoud 'Chollo' kulia mbele ya aliyekuwa kocha wa Simba SC, Mfaransa Patrick Liewig Mei 21, mwaka 2013 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Yanga SC ilishinda 2-0.

  Baada ya Nkongo kuenguliwa, Saanya atasaidiwa na Samuel Hudson Mpenzu wa Arusha, Josephat Daud Bulali wa Tanga, wakati mwamuzi wa akiba atakuwa Hashim Abdallah wa Dar es Salaam na Kamisaa wa mchezo huo ni Deogratius Rwechungura kutoka mkoani Mara.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: NKONGO ‘APIGWA CHINI’ YANGA NA AZAM, SASA MARTIN SAANYA KUKIPULIZA JUMAMOSI TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top