• HABARI MPYA

    Friday, August 28, 2015

    SIMBA, YANGA NA AZAM FC ZATAKIWA KUWASILISHA MIKATABA YA WACHEZAJI WOTE TFF

    KLABU za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zinatakiwa kuwasilisha mikataba ya wachezaji wake- nakala tatu kwa kila mchezaji kwa ajili ya kuidhinishwa na TFF, kama ilivyoelekezwa katika Kanuni ya 69(1) na (8).
    Baada ya mikataba hiyo kuidhinishwa ikiwa ni pamoja na kulipiwa ada ya sh. 50,000 kwa kila mmoja, nakala moja itakuwa ya klabu, nyingine ya mchezaji na moja itabaki TFF ili linapotokea tatizo la kimkataba uamuzi ufanywe na vyombo husika mara moja.
    Jonas Mkude katikati akisaini Mkataba wa Simba SC. Kulia Rais wa Simba SC, Evans Aveva na kushoto Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe

    Pia klabu ya VPL inatakiwa kuwasilisha TFF orodha ya benchi lake la ufundi, mikataba ya maofisa wa benchi husika pamoja na nakala za vyeti vyao. Kwa mujibu wa Kanuni ya 72 (3), Kocha Mkuu anatakiwa kuwa na Leseni ya CAF isiyopungua ngazi B wakati Kocha Msaidizi anatakiwa kuwa na Leseni ya CAF isiyopungua ngazi C.
    Kwa upande wa timu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL), Kocha Mkuu anatakiwa kuwa na Leseni ya CAF isiyopungua ngazi C wakati msaidizi anatakiwa kuwa na cheti kisichopungua ngazi ya Kati (Intermediate).
    Hakuna kocha asiyekidhi makatwa hayo ya kikanuni atakayeruhusiwa kuongoza timu yoyote kwenye mechi za ligi hizo mbili. Pia viongozi wa klabu wasiozingatia maelekezo haya, wanakumbushwa kuwa wanakwenda kinyume cha kanuni.
    Timu zinazoshiriki Ligi Kuu ni Ndanda FC, Mgambo Shooting, African Sports, Simba SC, Majimaji FC, JKT Ruvu, Azam FC, Prisons, Stand United, Mtibwa Sugar, Toto Africans, Mwadui, Mbeya City, Kagera Sugar, Yanga SC na Coastal Union.


    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA, YANGA NA AZAM FC ZATAKIWA KUWASILISHA MIKATABA YA WACHEZAJI WOTE TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top