• HABARI MPYA

  Ijumaa, Agosti 28, 2015

  MALINZI AFURAHIA KAMPUNI YA MADINI KUMWAGA UDHAMINI TIMU YA DARAJA LA KWANZA

  RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Jamal Malinzi (pichani kushoto) ameipongeza klabu ya Geita Gold SC inayoshiriki ligi Daraja la Kwanza nchini (FDL) kwa kupata udhamini wa shilingi milioni mia tatu (USD 150,000) toka kampuni ya uchimbaji madini ya Geita Gold Mining LTD.
  Katika salam zake za pongezi kwenda kwa uongozi wa klabu ya Geita, Malinzi ameipongeza klabu hiyo kwa hatua waliyofikia na zaidi kumshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Geita Gold Mining Terry Mullpeter kwa kuweza kuidhamini klabu hiyo.
  Aidha Malinzi amewaomba viongozi na wanachama wa klabu hiyo kuheshimu na kuenzi udhamini huo, kwa kuwa na nidhamu na kucheza vizuri ili kuweza kuendelea kuitangaza vyema Geita Gold Mining Limited.
  Malinzi ametoa wito kwa makampuni mengine kujitokeza na kuwekeza katika kudhamini vilabu vya ligi za madaraja ya chini ambazo hazina udhamini katika ligi zao, zikiwemo za daraja la kwanza, la pili, na mabingwa wa mikoa.
  Klabu ya Geita Gold SC inakuwa miongoni mwa timu chache zenye udhamini wa uhakika katika timu zinazoshiriki ligi daraja la kwanza mwaka huu miongoni mwa timu 24 zilizopo, ligi inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Septemba 19 mwaka huu, ikiwa kundi C pamoja na timu za Panone, JKT Oljoro, Polisi Mara, Mbao FC, Polisi Tabora na JKT Kanembwa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MALINZI AFURAHIA KAMPUNI YA MADINI KUMWAGA UDHAMINI TIMU YA DARAJA LA KWANZA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top