• HABARI MPYA

    Sunday, August 30, 2015

    MAMBO MAGUMU USAJILI SIMBA SC, DEMBELE AKATAA MAJARIBIO, NDAYISENGA NAYE ‘HASOMEKI’ TENA

    Na Princess Asia, ZANZIBAR
    WAKATI dirisha la usajili Tanzania linafungwa Saa 6:00 usiku wa leo, viongozi Simba SC wanaumiza vichwa jinsi ya kukamilisha zoezi hilo- hususan baada ya mshambuliaji kutoka Mali, Makan Dembele kugoma kufanya majaribio.
    Dembele ametua juzi Dar es Salaam na alitakuwa kuwasili Zanzibar tangu jana, lakini akachelewa na baada ya kufika akasema hawezi kufanya majaribio anataka ‘apewe chake’ asaini Mkataba aanze kazi.
    Wakala wake, Mganda Gibby Kalule alikuwa naye mchezaji huyo jukwaani Uwanja wa Amaan, Zanzibar jioni ya leo wakati Simba SC ikicheza mchezo wa kirafiki na Mafunzo na kushinda 3-1.
    Kocha Msaidizi wa Simba SC, Suleiman Matola amesema Dembele amekataa majaribio na benchi la Ufundi limesita kucheza ‘pata potea’ kwa mshambuliaji huyo wa zamani wa JS Kabyle ya Algeria.
    Mshambuliaji Makan Dembele (kushoto) akiwa na wakala wake Gibby Kalule (juu kulia) Uwanja wa Amaan, Zanzibar leo Simba SC ikimenyana na Mafunzo 

    Mshambuliaji mwingine aliyekuja kwa majaribio, Pape Abdoulaye N’daw kutoka Senegal leo amecheza mechi ya pili ya majaribio bila bao, baada ya jana pia kucheza Simba SC ikilala 2-0 mbele ya JKU.
    Lakini kwa N’daw inaonekana kama ni mchezaji ambaye akipewa muda anaweza kuja kuisaidia Simba SC kwa baadaye, kwani ni kijana mdogo, mrefu na anacheza kwa akili sana, kinachomkwamisha tu ni kutoelewana na wenzake uwanjani.
    Anaonekana ni mzuri kwa mipira ya juu si tu kwenye lango la adui hata kusaidia ulinzi mipira ya aina hiyo inapoelekzwa kwenye kango la timu yake.
    Aidha, pamoja na Simba SC kufanikiwa kufikia makubaliano na Mrundi, Kevin Ndayisenga, lakini kuna uwezekano usajili wake ukashindikana kutokana na muda mchache uliobaki.
    Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE kwamba tangu asubuhi wamekuwa wakihangaika kupata ndege ya kumuwahisha Ndayisenga Dar es Salaam aje kusaini.
    “Sijawasiliana na mtu aliyekuwa anashughulikia suala hilo, ila mara ya mwisho nchana walisema inakuwa shida kupata ndege ya kumuwahisha Ndayisenga Dar es Salaam, ila wanaendelea kulifanyia kazi,”alisema Poppe.
    Kumeibuka pia mpango mwingine wa kumrejesha mshambuliaji Mkenya Paul Kiongera kikosini. “Kuna wazo pia la kumrejesha Kiongera, kwa sababu tunaona kule kwao anacheza (KCB) na kufunga mabao, ila madaktari wetu hapa walituambia hayuko fiti,”amesema Poppe.
    Pape Abdoulaye N'daw akimtoka beki wa Mafunzo leo

    Mbali na Dembele, N’daw, Kiongera na Ndayisenga, wachezaji wengine wa kigeni Simba SC ni kipa Vincent Angban kutoka Ivory Coast, mabeki Emery Nimubona wa Burundi, Juuko Murushid, washambuliaji Simon Sserunkuma, Hamisi Kiiza wote wa Uganda na kiungo Justuce Majabvi wa Zimbabwe ambao wote wana mikataba tayari.
    Kanuni za usajili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara zinaruhusu wachezaji saba tu wa kigeni- maana yake Simba SC ina nafasi moja tu zaidi ambayo anaweza kuongezwa ama N’daw, Dembele, Kiongera au Ndayisenga.
    Kelvin Ndayisenga aliichezea Simba SC mechi moja tu dhidi ya URA na akafunga bao ikishinda 2-1
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAMBO MAGUMU USAJILI SIMBA SC, DEMBELE AKATAA MAJARIBIO, NDAYISENGA NAYE ‘HASOMEKI’ TENA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top