• HABARI MPYA

  Jumapili, Agosti 30, 2015

  ILIVYOTARAJIWA NI TOFAUTI NA ILIVYO SASA AKADEMI YA AZAM FC

  MAPEMA Mei mwaka 2012, Mwanasoka bora wa zamani Afrika, Abedi Ayew Pele ambaye pia ni Balozi wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), alizuru Tanzania na akapata fursa ya kuhudhuria mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Yanga na Azam.
  Kabla ya mchezo huo, Pele alitembelea mradi wa maendeleo ya soka ya vijana wa Azam FC, Chamazi, Dar es Salaam na akausifia sana, akisema utailetea matunda makubwa Tanzania baadaye.
  Na akasema Azam kwa ujumla, miaka kadhaa ijayo itakuwa klabu kubwa yenye hadhi sawa na Manchester United ya England kutokana na uwekezaji wake mzuri.
  Alisema akademi ya Azam ni nzuri na bora kuliko hata akademi yake. “Kwetu tuna akademi nyingi, lakini nyingi ni za wawekezaji wa nje (klabu za Ulaya), lakini hii ni ya Azam, safi sana. Akademi yangu ni ndogo tu, haiifikii hii kwa ubora, nami nina ndoto za kufanya kitu kama hiki, nadhani nitajifunza mengi kutoka kwa Azam,”alisema Pele.  
  Pele pia aliishauri Azam kuachana na desturi ya kuchukua wachezaji wa nje ya nchi, kwani kama wataitumia vizuri akademi yao kwa kusaka vipaji zaidi nchi mzima, mbele ya watu zaidi ya Milioni 40 watapata wachezaji bora.
  “Kama kwa lengo la kubadilishana tu uzoefu sawa, lakini kama una kademi nzuri kama hii, kwa nini uchukue mchezaji kutoka Ghana, hii nchi yenu ina watu zaidi ya Milioni 40, mnaweza kutengeneza wachezaji wengi wazuri na nyinyi mkauza Ulaya,”alisema Pele ambaye aliahidi kuanzisha ushirikiano wa akademi yake na ya Azam, baada ya kuombwa na aliyekuwa Rais wa TFF wakati huo, Leodegar Tenga.
  Pele pia aliizungumzia Ligi Kuu ya Tanzania baada ya kuona mechi ya Yanga ikiifunga Azam FC 2-0, akisema ina ubora sawa na ligi nyingine kubwa Afrika, ispokuwa tu inahitaji kuboreshwa.
  Kuhusu wachezaji, kulingana na alivyoona mechi ya Yanga na Azam, Pele alisema kwamba wana uwezo sawa na wachezaji wengi duniani na ili watimize ndoto za kucheza Ulaya, wanatakiwa kuongeza juhudi
  Mshambuliaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Ghana na klabu ya Olympique Marseille ya Ufaransa, pia aliwaambia wachezaji chipukizi wa Tanzania kwamba, hakuna njia ya mkato katika kutafuta mafanikio na kuwataka kufanya jitihada ili watimize ndoto zao.
  Pele, ambaye aliiongoza Marseille kutwaa ubingwa wa Ulaya mwaka 1992 akifunga moja ya mabao dhidi ya AC Milan ya Italia, alitembelea pia Kituo cha mafunzo ya soka kwa vijana wadogo Uwanja wa Karume, Ilala, Dar es Salaam ambayo huendeshwa siku za wikiendi kikihusisha watoto wa kuanzia umri wa miaka sita hadi 17.
  "Katika kufikia mafanikio hakuna njia ya mkato," alisema Pele ambaye aliletwa nchini FIFA kuangalia shughuli mbalimbali za maendeleo ya mpira wa miguu nchini.
  "Tunaona wachezaji wenye vipaji vikubwa duniani wakifanya jitihada kubwa ili waweze kucheza kwa kiwango cha juu. Bila ya kufanya juhudi, kujituma na kudhamiria huwezi kufanikiwa.
  "Wale wenye vipaji vikubwa, lakini hawafanyi jitihada watabakia. Wale wasiojaaliwa kuwa na vipaji vikubwa, lakini wanafanya jitihada, watakwenda mbele na kupata mafanikio," alisema nyota huyo wa Ghana ambaye alijijengea jina kwa kufunga mabao safi na muhimu kwa nchi yake na klabu ya Olympique Marseille wakati ikitamba katika soka barani Ulaya.
  Leo ni zaidi ya miaka mitatu sasa tangu Pele atue pale makao makuu ya Azam, maarufu kama Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam ni kuitabiria makubwa.
  Wakati huo, Mtendaji Mkuu wa sasa wa Azam FC, Saad Kawemba alikuwa anafanya kazi TFF na alihudhuria shughuli hiyo Chamazi- maana yake anakumbuka sana Pele alisema nini siku hiyo.
  Kwa mfano, Pele aliombwa na Tenga kushirikiana na akademi ya Azam FC na akasema yuko tayari, je tangu hapo jitihada gani zimefanyika kuhakikisha ushirikiano unakuwapo na unafanya kazi?
  Lakini pia, jitihada gani zimefanyika tangu hapo kuifanya akademi ya Azam FC iwe kubwa japo kwa Afrika pekee? Kwa sasa hakuna mashindano ya Kombe la Uhai, na vijana wa Azam FC hawashiriki mashindano ya mtaani- maana yake zaidi ya kucheza mara moja moja mechi za utangulizi wakati wa Ligi Kuu, hakuna cha ziada.
  Kuna mashindano mengi ya vijana ya kila mwaka yanafanyika nchi mbalimbali za Ulaya, jitihada gani zimefanyika kuhakikisha Azam akademi inashiriki?
  Mmoja wa Wakurugenzi wa Azam FC, Yussuf Bakhresa mwanzoni mwa miaka ya 2000 alikuwa anakwenda na timu za vijana nchi za Scandinavia kwenye mashindano.
  Kocha wa zamani wa Simba SC, Aluko Ramadhani pia alikuwa anakwenda na timu yake ya vijana nchi za Scandivania na kuna wakati viungo wa zamani wa Azam FC, Ramadhani Chombo ‘Redondo’ na Jabir Aziz walipata timu huko, bahati mbaya wenyewe wakaamua kurudi nyumbani. 
  Lakini tunafahamu kuna timu za vijana huenda Ujerumani mara kwa mara kucheza mashindano, je Azam FC wamekwishawahi kujishughulisha kupata fursa hizo kupeleka timu yao?
  Kama jitihada za aina hiyo hakuna, ni vipi ndoto za Pele kuiona akademi ya Azam FC inakuwa Afrika zitatimia?
  Nchi za wenzetu hapa Afrika pekee, zina akademi imara, je, Azam FC wamekwishawahi kufikiria hata mara moja japo kuwasafirisha vijana wake kwenda kucheza na vijana wenzao mfano wa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, TP Mazembe ya DRC au ASEC?
  Rais wa sasa wa TFF, Jamal Malinzi amewapatia nafasi za kujiunga na akademi ya Orlando Pirates wachezaji watano wa chini ya umri wa miaka 15,  Asaad Ali Juma wa Zanzibar, Maziku Aman, Issa Abdi wa Dodoma, Kelvin Deogratias wa Geita na Athumani Maulid wa Kigoma baada ya mazungumzo na Rais wa klabu hiyo, Irvin Khoza. Na makubaliano ni kwamba vijana hao watafanyiwa majaribio, ambayo wakifuzu, watajiunga na timu ya vijana ya Orlando Pirates.
  Inavyoonekana sasa akademi ya Azam FC imepoteza mwelekeo kutokana na kukosa watu maalum wa kuisimamia na kufanywa kuwa sehemu tu ya Azam FC, kitu ambacho si sawa.
  Vyema sasa, bodi ya Ukurugenzi ya Azam FC, uongozi na watendaji wakarejea maneno ya Abedi Pele na kufikiria namna ya kuifanya akademi yao iwe kweli ya kimataifa, maana sasa hali ilivyo ni tofauti ilivyotarajiwa. Leo nimeamka hivyo. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ILIVYOTARAJIWA NI TOFAUTI NA ILIVYO SASA AKADEMI YA AZAM FC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top