• HABARI MPYA

  Jumatatu, Agosti 24, 2015

  PAMOJA NA KUIKOSA NGAO, LAKINI AZAM FC YAWEKA REKODI YA KIPEKEE HAIJAWAHI KUTOKEA

  Kipa wa Azam FC, Aishi Manula akiwa amedaka mpira mbele ya Nahodha wa Yanga SC, Nadir Haroub 'Cannavaro' Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam

  REKODI YA STEWART TANGU AREJEE AZAM

  Azam FC 4-2 Friends Rangers (Kirafiki Chamazi)
  Azam FC 1-0 JKT Ruvu (Kirafiki Chamazi)
  Azam FC 1-0 African Sports (Kirafiki Tanga
  Azam FC 1-0 Coastal Union (Kirafiki Tanga)
  Azam FC 1-0 KCCA (Kagame Taifa)
  Azam FC 2-0 Malakia (Kagame Taifa)
  Azam FC 5-0 Adama City (Kagame Taifa)
  Azam FC 0-0 Yanga SC (pen5-3, Robo Fainali Kagame Dar)
  Azam FC 1-0 KCCA (Nusu Fainali Kagame Dar)
  Azam FC 2-0 Gor Mahia (Fainali Kagame)
  Azam FC 1-0 KMKM (Kirafiki Zanzibar)
  Azam FC 3-0 Mafunzo (Kirafiki Zanzibar)
  Azam FC 2-0 JKU (Kirafiki Zanzibar)
  Azam FC 0-0 Yanga SC (7-8 penalti Ngao ya Jamii)
  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  JUMAMOSI Azam FC ilishindwa kwa penalti 8-7 na Yanga SC katika mchezo wa Ngao ya Jamii, lakini kocha Muingereza Stewart John Hall alifurahia kuiongoza timu hiyo kwa mara ya 13 mfululizo bila nyavu zake kuguswa.
  Dakika 90 ziliisha kwa sare ya 0-0 kabla ya kipa, Ally Mustafa Mtinge ‘Barthez’ kupangua penalti za beki raia wa Ivory Coast, Serge Wawa Pascal na mshambuliaji Ame Ali ‘Zungu’ na kuipa Yanga SC Ngao ya tatu mfululizo dhidi ya Azam FC.
  Lakini Stewart alikamilisha mechi ya 13 kucheza bila nyavu za timu yake kuguswa tangu arejee Azam FC Juni mwaka huu- rekodi ambayo ni ya kipekee kabisa.
  Ni Friends Rangers pekee walioweza kuupenya ukuta wa Azam FC ya Stewart na kufunga mara mbili wakilala 4-2 katika mchezo wake wa kwanza kabisa wa kirafiki Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Baada ya hapo, Azam FC ilishinda 1-0 dhidi ya JKT Ruvu Chamazi, 1-0 dhidi ya African Sports Tanga, 1-0 dhidi ya Coastal Union Tanga, zote zikiwa mechi za kirafiki kabla ya kuingia Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame na kushinda mechi zote hadi kutwaa ubingwa.
  Ilianza kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya KCCA kabla ya kuzifunga 2-0 Malakia ya Sudan Kusini, 5-0 Adama City ya Ethiopia na baadaye kushinda kwa penalti 5-3 dhidi ya Yanga SC baada ya sare ya 0-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Katika Nusu Fainali, Azam FC iliichapa tena 1-0 KCCA kabla ya kumaliza kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya 2-0 Gor Mahia ya Kenya katika Fainali na kutwaa Kombe la Kagame kwa mara ya kwanza.
  Azam FC imecheza mechi 13 bila nyavu zake kuguswa
  Kutoka hapo, Azam FC ikashinda mechi tatu mfululizo za kirafiki visiwani Zanzibar 1-0 dhidi ya KMKM, 3-0 dhidi ya Mafunzo na 2-0 dhdi ya JKU kabla ya sare ya 0-0 na Yanga SC katika mechi ya Ngao- ambayo mwishowe walifungwa kwa penalti 8-7.
  Kipa wa Azam FC, Aishi Manula alicheza penalti ya kwanza ya Yanga SC iliyopigwa na Nahodha wao, Nadir Haroub Ali ‘Cannavaro’ lakini Wawa akaenda kukosa kabla ya Ame pia kukosa.
  Penalti za Yanga SC zilifungwa na Haruna Niyonzima, Deus Kaseke, Amissi Tambwe, Andrey Coutinho, Godfrey Mwashiuya, Thabani Kamusoko, Mbuyu Twite na Kelvin Yondan aliyepiga ya mwisho.
  Penalti za Azam FC zilifungwa na Kipre Herman Tchetche, Nahodha John Raphael Bocco, Himid Mao Mkami, Aggrey Morris, Jean Baptiste Mugiraneza, Erasto Nyoni na Shomary Kapombe. 
  Kocha Stewart Hall ameweka rekodi ya kipekee Azam FC
  Ni mara ya tano sasa Yanga SC kutwaa Ngao ya Jamii ikiwa ni rekodi, baada ya kuifunga Simba SC mara mbili, mwaka 2001 mabao 2-1 na 2010 kwa penalti 3-1 baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika ya 90, kabla ya kuifunga Azam FC miaka mitatu mfululizo, 2013 bao 1-0 na 2014 mabao 3-0.
  Inafuatia Simba SC iliyotwaa Ngao mara mbili, mwaka 2011 wakiifunga Yanga SC 2-0 na 2012 wakiifunga Azam FC 3-2, wakati Mtibwa Sugar ni timu nyingine iliyowahi kutwaa Ngao mwaka 2009 ikiifunga 1-0 Yanga SC.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: PAMOJA NA KUIKOSA NGAO, LAKINI AZAM FC YAWEKA REKODI YA KIPEKEE HAIJAWAHI KUTOKEA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top