• HABARI MPYA

  Alhamisi, Agosti 27, 2015

  PINTO MWENYEKITI MPYA KAMATI YA MISS TANZANIA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MWENYEKITI wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), Juma Pinto, jana ametangazwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati mpya itakayosimamia shindano la urembo la Taifa (Miss Tanzania).
  Akitangaza Kamati hiyo leo kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo), Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino Agency International, Hashim Lundenga, alisema kwamba kamati hiyo ndiyo itasimamia mchakato wote wa shindano hilo kwa kufuata mwongozo utakaotolewa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata).
  Lundenga alimtaja Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo ni Lucas Rutta, Katibu ni Doris Mollel ambaye alikuwa mshindi wa tatu wa shindano hilo mwaka juzi huku Jokate Mwegelo, atakuwa Msemaji wa Kamati hiyo.

  Aliwataja wajumbe kuwa ni pamoja na Miss Tanzania mwaka 1999, Hoyce Temu, Mohammed Bawazir, Gladyz Shao, Magdalena Munisi, Shah Ramadhan, Hamm Hashim, Khalfan Saleh na Ojambi Masaburi.
  Lundenga aliwataja wajumbe wengine wataounda sekretarieti ya Kamati hiyo ni wanne ambao ni Dk. Ramesh Shah, Hidan Ricco, Yasson Mashaka na Deo Kapiteni.
  Mara baada ya kutangazwa, Pinto, alisema kuwa wanashukuru kwa kupata nafasi hiyo na wanaahidi wataendesha vyema shindano hilo.
  " Ikionekana mtu ameenda kinyume na taratibu, atafukuzwa, hakuna kitu kibaya kama kuvunja miiko ya mashindano haya", Lundeng alisisitiza.
  Pinto alisema kwamba wanafahamu changamoto zilizojitokeza katika shindano hilo na watajiandaa kufanya mashindano yatakayoleta tafsiri sahihi ya maana halisi ya urembo na malengo.
  Jokate alisema kuwa mashindano hayo yamewasaidia warembo kupata fursa mbalimbali za kujiendeleza akiwamo yeye.
  "Tutafanya juu chini kuhakikisha tunarudisha hadhi ya shindano hilo, tutafanya mashindano yenye hadhi ya kisasa kama yanayofanyika kwenye nchi zilizoendelea", alisema mshindi huyo wa pili wa Miss Tanzania mwaka 2006.
  Aliongeza kwamba wanataka kufanya shindano lenye sura mpya na wanawaahidi wadau wa sanaa hiyo ya urembo sasa washiriki wote watakuwa kwenye mikono salama.
  "Tutafanya shindano kwa kufuata miiko ya shindano", alisema.
  Kamati hiyo inatarajia kutangaza mchakato mpya wa shindano la mwaka huu na maandalizi ya mwakilishi wa Tanzania kwenye fainali za Miss World zitakazofanyika baadaye mwaka huu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: PINTO MWENYEKITI MPYA KAMATI YA MISS TANZANIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top