• HABARI MPYA

    Friday, August 28, 2015

    MSENEGALI WA SIMBA SC ‘KIKAANGONI’ KESHO, YULE DEMBELE WA MALI LABDA ATAWASILI LEO

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI kutoka Pape Abdoulaye N’daw kesho atafanyiwa mtihani wa kwanza wa majaribio wakati Simba SC itakapomenyana na Mafunzo Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
    Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba N’daw aliyetokea klabu ya Dinamo Bucuresti ya Ligi Kuu ya Romania atacheza pia mechi nyingine Jumapili dhidi ya JKU.
    “Baada ya mechi hizo mbili, naamini benchi la Ufundi litakuwa limeona uwezo wake na kuamua kama asajiliwe au aachwe aende,”amesema Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ). 

    Pape Abdoulaye N’daw kesho atafanyiwa mtihani wa kwanza wa majaribio wakati Simba SC itakapomenyana na Mafunzo Uwanja wa Amaan, Zanzibar

    Kuhusu mchezaji kutoka Mali, Makan Dembele, Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Usajili ya Simba SC amesema kwamba anatarajiwa kuwasili leo. “Kumekuwa na vikwazo katika safari yake, lakini tunadhani leo atafika,”amesema kuhusu mchezaji huyo kutoka JS Kabylie ya Algeria.
    Wawili hao wanakuja baada ya Simba SC kuachana na Msenegali mwingine, Papa Niang kufuatia kumjaribu kwa dakika 45 tu Jumamosi iliyopita katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Mwadui FC ya Shinyanga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam timu hizo zikitoka 0-0.
    Niang alikuja Simba SC baada ya klabu hiyo kushindwa kufikia makubaliano na mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Kevin Ndayisenga juu ya dau la usajili.
    Niang aliyetoka Alianza F.C. ya El Salvador ambaye ni mdogo wa mshambuliaji wa kimataifa wa zamani wa Senegal, Mamadou Niang Jumamosi alishindwa kabisa kuwashawishi wana Simba kwa soka yake duni.
    Mchezaji huyo wa zamani wa CF Mounana ya Gabon, Al Shabab SC ya Kuwait, FC Vostok ya Kazakhstan, FF Jaro, AC Oulu na FC OPA za Finland aliondoka usiku wa Jumamosi kurejea kwao, ikiwa ni baada ya siku tatu za kuwa Dar es Salaam.
    Awali Simba SC pia ilishindwa kumsajili mshambuliaji mwingine hatari wa Vital’O, Laudit Mavugo kufuatia klabu mbili za nchini humo kupandisha thamani ya mchezaji huyo na kuwa Sh. Milioni 200, badala 110 walizokubaliana awali.
    Aidha, kuibuka pia kwa mzozo mpya kati ya klabu ya Vital’O FC na Solidarity FC, inayodai kumlea Mavugo na kudai ina hakimiliki ya mchezaji huyo nako kuliishitua Simba.
    Vital’O ikaikoroga zaidi Simba SC baada ya kudai kiwepo kipengele cha wao kupata asilimia 50 kama mchezaji huyo atauzwa na Wekundu hao wa Msimbazi kwenda klabu nyingine.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MSENEGALI WA SIMBA SC ‘KIKAANGONI’ KESHO, YULE DEMBELE WA MALI LABDA ATAWASILI LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top