• HABARI MPYA

  Jumapili, Agosti 30, 2015

  SIMBA SC YAREJESHA HESHIMA ZANZIBAR, YAITANDIKA 3-1 MAFUNZO, KIIZA ANG’ARA

  Mshambuliaji Mganda Hamisi ‘Diego’ Kiiza akishangilia baada ya kufungia Simba SC bao la tatu dhidi ya Mafunzo leo

  Na Princess Asia, ZANZIBAR
  SIMBA SC imerejesha heshima baada ya kuibuka na ushindi wa maabo 3-1 dhidi ya Mafunzo katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar jioni ya leo. 
  Kocha Muingereza, Dylan Kerr alifanya mabadiliko langoni mwake leo akimuanzisha kipa Peter Manyika badala ya Vincent Angban aliyedaka jana timu ikifungwa 2-0 na JKU. 
  Mafunzo walikuwa wa kwanza kupata bao, lililofungwa na Jaku Joma dakika ya 30 baada ya kupokea pasi ya Haji Ramadhani n kumtoka beki Said Issa kabla ya kumchambua kipa Manyika.
  Simba SC ikasawazisha bao hilo kupitia kwa Peter Mwalyanzi dakika ya 36 kufuatia pasi ya Daniel Lyanga aliyesaidiana naye kuipasua ngome ya Mafunzo.
  Beki Said Issa akasawazisha makosa yake baada ya kuruke vizuri hewani kumalizia kwa kichwa mpira wa adhabu ulipigwa na kiungo Awadh Juma Issa dakika ya 43.
  Kipindi cha Simba SC ilianza na mabadiliko ikimtoa Lyanga na kuingia Mganda Hamisi ‘Diego’ Kiiza aliyekwenda kufunga bao la tatu dakika ya 68 baada ya pasi nzuri ya Mwinyi Kazimoto. 
  Kwa mara nyingine mshambuliaji kutoka Senegal, Pape Aboulaye N’daw leo alishindwa kuwafurahisha mashabiki kama jana alipocheza mechi ya kwanza ya majaribio Simba SC ikifungwa 2-0 na JKU.
  Said Issa akiruka juu kuifungia kwa kichwa Simba SC bao la pili


  Mfungaji wa bao la kwanza la Simba SC, Peter Mwalyanzi akimtoka beki wa Mafunzo, Hajji Ramadhani

  Mshambuliaji Msenegali wa Simba SC, Pape Abdoulaye N'daw akiruka juu kupiga kichwa dhidi ya beki wa Mafunzo, Said Yussuf

  Kiungo wa Simba SC, akimtoka beki wa Mafunzo, Hassan Ahmada

  N’daw alikaribia kufunga dakika ya 72 baada ya kuunganishia juu ya lango kwa kichwa krosi ya Hassan Kessy na dakika ya 75 akatolewa kumpisha chipukizi Issa Ngoa.
  Simba SC imeweka kambi visiwani kujiandaa na Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inayotarajiwa kuanza Septemba 12 mwaka huu, wakifungua dimba na African Sports mjini Tanga.
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Peter Manyika, Hassan Kessy, Samih Haji Nuhu, Said Issa, Justuce Majabvi, Awadh Juma, Mwinyi Kazimoto/Simon Sserunkuma dk75, Mussa Mgosi/Joseph Kimwaga dk60, Peter Mwalyanzi, Pape Abdoulaue N’daw/Issa Ngoa dk80 na Danny Lyanga/Hamisi Kiiza dk46. 
  Mafunzo FC; Hashim Haroun, Juma Othman, Abdulrahim Abdallah/Sadik Habib dk38, Kheri Salum, Haji Ramadhan, Hassan Ahmada, Mohamed Abdulrahman, Abdulaziz Makame, Jaku Juma na Ali Juma Hassan. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAREJESHA HESHIMA ZANZIBAR, YAITANDIKA 3-1 MAFUNZO, KIIZA ANG’ARA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top