• HABARI MPYA

  Jumatano, Agosti 26, 2015

  SIMBA SC HAWAWAJUI VIZURI WACHEZAJI WA BURUNDI, SHAURI YAO, BURE AGHALI!

  SIMBA SC imemsafirisha kurudi kwao, mshambuliaji Msenegali, Papa Niang mara baada tu ya kumjaribu kwa dakika 45 juzi katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Mwadui FC ya Shinyanga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Wakati mdogo huyo wa mshambuliaji wa zamani wa kimataifa wa Senegal, Mamadou Niang akiwa njiani kurejea kwao baada ya siku tatu za kuwa nchini, ‘nduguye’, Msenegali mwingine Pape Abdoulaye N'Daw alikuwa njiani kuja Dar es Salaam.
  Inaelezwa Msenegali huyo mwingine tayari yupo nchini pamoja na mshambuliaji mwingine kutoka Mali kwa ajili ya majaribio.
  N'Daw mwenye umri wa miaka 21, wasifu wake unasema kwa sasa anachezea klabu ya Liga Kuu ya Romania, Dinamo Bucuresti, wakati wa Mali bado jina lake halijapatikana na haijulikani anatoka timu gani. 
  Ikumbukwe Niang alikuja Simba SC baada ya klabu hiyo kushindwa kufikia makubaliano na mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Kevin Ndayisenga juu ya dau la usajili.
  Niang kutoka klabu ya Alianza F.C. ya El Salvador alishindwa kabisa kuwashawishi wana Simba kwa soka yake akicheza mechi ya kirafiki na Mwadui FC ya kocha Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.
  Paul Nonga wa Mwadui alionekana mshambuliaji bora zaidi kuliko mchezaji wa Senegal, Niang ambaye wasifu wake unasema amechezea CF Mounana ya Gabon, Al Shabab SC ya Kuwait, FC Vostok ya Kazakhstan, FF Jaro, AC Oulu na FC OPA za Finland.
  Awali Simba SC pia ilishindwa kumsajili mshambuliaji mwingine wa Burundi, Laudit Mavugo kufuatia klabu mbili za nchini humo kupandisha thamani ya mchezaji huyo na kuwa Sh. Milioni 200, badala 110 walizokubaliana awali.
  Aidha, kuibuka pia kwa mzozo mpya kati ya klabu ya Vital’O FC na Solidarity FC, inayodai kumlea Mavugo na kudai ina hakimiliki ya mchezaji huyo nako kuliishitua Simba.
  Vital’O ikaikoroga zaidi Simba SC baada ya kudai kiwepo kipengele cha wao kupata asilimia 50 kama mchezaji huyo atauzwa na Wekundu hao wa Msimbazi kwenda klabu nyingine.   
  Ikumbukwe mwezi huu Simba SC ilimuuza mshambuliaji wake mahiri, Mganda Emmanuel Arnold Okwi klabu ya SonderjyskE FC ya Ligi Kuu ya Denmark kwa dola za Kimarekani 110,000 (Sh. 220).
  Simba SC ilimjaribu Ndayisenga katika mchezo wa kirafiki dhidi ya URA ya Uganda wiki iliyopita na akacheza vizuri na kufunga bao timu hiyo ikishinda 2-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
  Lakini siku chache baadaye akapanda ndege kurejea kwao Burundi baada ya Simba SC kushindwa kufika gharama za manunuzi yake, ambayo si zaidi ya dola 50,000 jumla kwa gharama halisi (Sh. Milioni 100).
  Kuondoka kwa Ndayisenga kuliwasikitisha mno wana Simba SC, kwani mchezaji huyo aliwasisimua mashabiki wa timu hiyo ya Msimbazi kwa soka yake nzuri na kuanza kutamba wamepata ‘kifaa’ cha kuwaadabisha wapinzani.
  Niliandika Jumapili kwamba Simba SC wanafanya makosa kumuacha Ndayisenga ambaye amewadhihirishia maelfu ya mashabiki wa timu hiyo ni mchezaji mzuri. 
  Na baada ya Simba SC kupokea Sh. Milioni 220 kwa kumuuza Okwi, jiulize wanashindwaje kutumia nusu ya fedha hizo kununua mchezaji mwingine ambaye anaonekana anaweza kuwa tishio kama Okwi?
  Kiongozi mmoja wa Simba SC aliniambia hawawezi kumnunua mchezaji wa Burundi kwa fedha nyingi kiasi hicho hazilingani na thamani yake, akitolea mfano Amisi Tambwe walimnunua kwa bei ndogo kabla hajahamia Yanga SC.
  Nilichekea ‘mbavuni’ tu, nikaona kweli Simba SC hawajui thamani ya wachezaji wa Burundi. Nitawaeleza kwa uchache. 
  Saido Berahino wengi tunamjua, anachezea West Bromwich Albion ya Ligi Kuu England, huyu ni Mrundi ambaye sasa amekuwa raia wa Uingereza.
  Berahino alizaliwa Bujumbura, ambako alianzia soka na baada ya baba yake kuuawa mwaka 1997 katika vita vya wenyewe kwa wenyewe Burundi akaenda England mwenyewe akiwa na umri wa miaka 10 kumfuata mama yake, aliyekuwa anaishi na wanawe wengine wa kiume na wa kike mjini Newtown, Birmingham. 
  Alipata misukosuko kidogo baada ya kuwasili England ikiwemo kuwekwa chini ya uangalizi kwanza hadi vipimo vya DNA vithibitishe ni mtoto kweli wa mama huyo aitwaye Liliane.
  Berahino akaingia shule ya Aston Manor ambako pamoja na kuhitimu vizuri masomo yake alifanya vizuri katika michezo ya Riadha, mpira wa kikapu na soka. 
  Berahino akachukuliwa na akademi ya soka ya West Brom na ‘alipoiva’ akaanza kutolewa kwa mkopo kwenda kupata uzoefu akichezea klabu za Northampton Town 2011, Brentford 2012 na Peterborough United kabla ya kurejea WBA mwaka 2013 na sasa anang’ara.
  Huyu sasa ni mchezaji wa timu za vijana za England, ambaye anaweza kuchezea timu ya taifa ya wakubwa ya Burundi akitaka.
  Na kama kweli anataka kucheza soka ya kimataifa, Berahino atalazimika tu kuamua kuchezea Burundi, kwa sababu ni vigumu mno kwake kupata nafasi Three Lions.
  Ni orodha ndefu ya vipaji vya Warundi kuanzia wale ambao waliwika hapa miaka ya nyuma kama Nonda Shabani aliyecheza pia Ulaya, Constantine Kimanda, Ngandou Ramadhani, Ramazani Wasso, Mwinyi Rajab, Suleiman Ndikumana na wengineo. 
  Kwa Warundi wanaotamba sasa Ulaya, kuna mtu pia anaitwa Jonathan Nanizayamo mzaliwa wa Ufaransa, ambaye anachezea Lens ya Ufaransa baada ya kuchezea, Real Sociedad ya Hispania, iliyomkuza kuanzia akademi.
  Katikati ya mwaka huu, wakala Dennis Kadito aliyetaka kuwauzia Simba SC Ndayisenga, alifanikisha dili na Mrundi mwingine, Abdul Razak Fiston kununuliwa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kwa Sh. Milioni 500 kutoka klabu ya Sofapaka ya Kenya.
  Ni Kadito huyo huyo aliyewahi kumpeleka Shomary Kapombe Ufaransa kutoka Simba SC kwenda AS Cannes ya Daraja la Nne nchini humo akimuhakikishia atafika Ligi kubwa baada ya uvumilivu wa muda.
  Lakini baada ya miezi michache Kapombe alirejea Tanzania na kujiunga na Azam FC- kwa sasa Kadito hana hamu na wachezaji wa Tanzania baada ya kitendo cha Kapombe na amehamishia msaada wake kwa wachezaji wengine wa nchi jirani wenye nia kweli ya kucheza soka ya kulipwa nchi zenye kutoa maslahi mazuri. 
  Lengo ni kuwaeleza Simba SC kuhusu thamani ya wachezaji wa Burundi- ili waone dola 50,000 si kitu kwa mchezaji kama Ndayisenga ambaye yupo mikononi mwa wakala makini, Kadito. 
  Kwa ninavyofahamu, mchezaji anapokwenda majaribio lazima awe na barua ya mwaliko na agharimiwe tiketi, malazi, chakula na usafiri wa ndani anapokuwa kwenye majaribio.
  Maana yake Simba SC iliingia gharama za aina hiyo kwa Ndayisenga, Niang na sasa hawa wawili wa Senegal na Mali waliokuja.
  Unaweza kukuta gharama za tiketi, chakula, malazi na usafiri wa ndani ilizotumia Simba SC hadi sasa kuleta wachezaji kwa majaribio hazifiki fedha ambazo ingeongeza wangempata Ndayisenga. Hiyo ndiyo waswahili wanasema; “Bure aghali”. Alamsiki. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC HAWAWAJUI VIZURI WACHEZAJI WA BURUNDI, SHAURI YAO, BURE AGHALI! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top