• HABARI MPYA

    Wednesday, August 26, 2015

    DEMBELE LA MALI LATUA SIMBA SC KWA MAJARIBIO

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Mali, Makan Dembele amewasili nchini kwa majaribio ya kujiunga na klabu ya Simba SC.
    Makan na mshambuliaji mwingine aliyekuja kwa majaribio jana Pape Abdoulaye N’daw kutoka Dinamo Bucuresti ya Romania, wamekwenda Zanzibar ambako timu hiyo imeweka kambi kwa maandalizi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba Dembele aliyezaliwa Desemba 25, mwaka 1986 kwa sasa anachezea klabu ya JS Kabylie ya Algeria.
    Makan Dembele akiichezea JS Kabyle ya Algeria, amekuja Simba SC kwa majaribio

    Wawili hao wanakuja baada ya Simba SC kuachana na Msenegali mwingine, Papa Niang kufuatia kumjaribu kwa dakika 45 tu Jumamosi katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Mwadui FC ya Shinyanga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam timu hizo zikitoka 0-0.
    Niang alikuja Simba SC baada ya klabu hiyo kushindwa kufikia makubaliano na mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Kevin Ndayisenga juu ya dau la usajili.
    Niang aliyetoka Alianza F.C. ya El Salvador ambaye ni mdogo wa mshambuliaji wa kimataifa wa zamani wa Senegal, Mamadou Niang Jumamosi alishindwa kabisa kuwashawishi wana Simba kwa soka yake duni.
    Mchezaji huyo wa zamani wa CF Mounana ya Gabon, Al Shabab SC ya Kuwait, FC Vostok ya Kazakhstan, FF Jaro, AC Oulu na FC OPA za Finland aliondoka usiku wa Jumamosi kurejea kwao, ikiwa ni baada ya siku tatu za kuwa Dar es Salaam.
    Awali Simba SC pia ilishindwa kumsajili mshambuliaji mwingine hatari wa Vital’O, Laudit Mavugo kufuatia klabu mbili za nchini humo kupandisha thamani ya mchezaji huyo na kuwa Sh. Milioni 200, badala 110 walizokubaliana awali.
    Aidha, kuibuka pia kwa mzozo mpya kati ya klabu ya Vital’O FC na Solidarity FC, inayodai kumlea Mavugo na kudai ina hakimiliki ya mchezaji huyo nako kuliishitua Simba.
    Vital’O ikaikoroga zaidi Simba SC baada ya kudai kiwepo kipengele cha wao kupata asilimia 50 kama mchezaji huyo atauzwa na Wekundu hao wa Msimbazi kwenda klabu nyingine.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: DEMBELE LA MALI LATUA SIMBA SC KWA MAJARIBIO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top