• HABARI MPYA

    Monday, August 31, 2015

    ZITTO KABWE ATAKA MASHABIKI WAINGIE BURE MECHI YA TAIFA NA NIGERIA JUMAMOSI TAIFA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KIONGOZI wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, amelitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutangaza kutotoza kiingilio chochote katika mchezo wa kuwania tiketi ya kushiriki fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kati ya wenyeji Taifa Stars dhidi ya Nigeria (Super Eagles).
    Taifa Stars ambao wameweka kambi nchini Uturuki wanatarajia kuikaribisha Super Eagles Jumamosi Septemba 5 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
    Akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni za uchaguzi zilizofanyika jana viwanja vya Zakhem Mbagala, Zitto, alisema kuwa mechi hiyo ni nyeti na Taifa Stars inahitaji kushinda ili kurejesha mazingira ya kufuzu mashindano hayo yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

    Zitto alisema kuwa kutokana na Taifa Stars kupoteza mechi ya kwanza kwa kufungwa mabao 3-0 na Misri, timu hiyo inahitaji kushinda mchezo wake wa hapa nyumbani hapo Jumamosi.
    Alisema kwamba hakuna timu inayokata tiketi ya kushiriki mashindano makubwa kama haijashinda mechi zake za nyumbani.
    "Tuna mpango wa kuhakikisha tunashiriki Kombe la Dunia kabla ya mwaka 2025", alisema Zitto.
    Kiongozi huyo aliyehamia kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) aliwataka Watanzania wasiwapigie kura viongozi ambao hawaonekani viwanjani kwa sababu hawatasaidia maendeleo ya mchezo huo wa soka.
    "Jumamosi wote tukutane Uwanja wa Taifa ili tuifunge Nigeria", alimaliza kiongozi huyo ambaye ni mwanachama wa Klabu ya Simba na ambaye hujitokeza mara kwa mara kuishangilia timu yake au Taifa Stars inapocheza kwenye viwanja mbalimbali ndani na nje ya nchi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ZITTO KABWE ATAKA MASHABIKI WAINGIE BURE MECHI YA TAIFA NA NIGERIA JUMAMOSI TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top